Mhubiri: Askofu Charles Kariuki – Kutoka Kenya
MAANDIKO: Ezekieli 37:1-13

“Mkono wa Bwana ulikuwa juu yangu, naye akanichukua nje katika roho ya Bwana, akaniweka chini, katikati ya bonde; nalo limejaa mifupa; akanipitisha karibu nayo pande zote; na tazama, palikuwa na mifupa mingi katika ule uwanda! Nayo, tazama, ilikuwa mikavu sana. Akaniambia, Mwanadamu, je! Mifupa hii yaweza kuishi? Nami nikajibu, Ee Bwana MUNGU, wajua wewe.”

UTANGULIZI

Wapendwa katika Bwana.
Leo tunajifunza kuhusu Bonde la Mifupa Mikavu, ujumbe wa kinabii unaotufundisha juu ya hali ya kanisa na nafasi ya waamini mbele za Mungu.

Katika maono haya, Nabii Ezekieli anawekwa katikati ya bonde lililojazwa mifupa mikavu. Mifupa hii haikuwa ya wageni, bali ilikuwa ni ya nyumba ya Israeli watu wa Mungu waliokuwa wamepoteza uhai wa kiroho.
Israel katika Agano la Kale inawakilisha Kanisa la Mungu, na mifupa hiyo inawakilisha waamini waliokauka kiroho.

BONDE LA MIFUPA MIKAVU – HALI YA KANISA

Bonde hili lilikuwa limejaa mifupa iliyosambaa kila mahali, mifupa mikavu, isiyo na tumaini.
Swali la Bwana lilikuwa:

“Mwanadamu, je! Mifupa hii yaweza kuishi?”

Ezekieli alijibu kwa unyenyekevu:

“Ee Bwana Mungu, wajua wewe.”

Hii ni picha ya kanisa lililopoteza uhai wa kiroho kanisa lililoko bondeni badala ya kuwa mlimani.
Kanisa halikupaswa kuwa kavu, halikupaswa kuwa bondeni; lilipaswa kuwa hai, lenye Roho, lenye nguvu, na lenye utukufu wa Mungu.

Lakini kwa nini kanisa liko katika hali hii?
Ni kwa sababu kanisa limepoteza ukomavu wake na kutoka katika nafasi yake halisi ya kiroho.

MPANGO WA MUNGU KWA KANISA

Mungu hana mpango wa kukaa na kanisa lililokufa;
Anataka kanisa lililo hai, lililokomaa, lenye uwezo wa kutawala duniani.

Yesu alisema:

Mathayo 16:18 “Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.”

Yesu ndiye mjenzi wa kanisa lake.
Kanisa linapitia hatua za ujenzi kutoka utoto wa kiroho hadi ukomavu wa kiroho.
Na lengo la Mungu ni kuwa na kanisa lililokamilika, lenye mamlaka na lenye uwezo wa kutawala katika ulimwengu huu.

KUSIMAMA KATIKA NAFASI YAKO

Mungu amesema:

“Unapaswa kukaa katika nafasi yako.”

Hii ni kauli kutoka mbinguni, ikimaanisha kuwa wewe siyo mtoto tena.
Kwa maana mtoto hawezi kumilikishwa urithi wa Baba yake.
Lakini sasa wewe ni kanisa lililokomaa, na Mungu amekupa mamlaka ya kusimama katika nafasi yako ili umiliki.

Sasa ni wakati wa kanisa kukomaa kiroho.
Siyo wakati wa kukaa kimya, bali wakati wa kusimama na kutangaza utukufu wa Mungu.
Ufalme wa Mungu unahitaji watu waliokomaa watu wanaojua nafasi zao, wanaosimama imara katika wokovu na haki.

Yesu mwenyewe alitoa mfano wa ukomavu.
Alipokuwa mdogo, kabla ya kufikia miaka thelathini (30), hakuchukua umiliki wowote wa kiroho.
Lakini alipotimiza miaka thelathini, akaenda Mto Yordani na kubatizwa na Yohana.

Ndipo sauti ikasikika kutoka mbinguni ikisema:

Mathayo 3:17 “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye.”

Hiyo ilikuwa ni ishara ya ukomavu wa kiroho.
Nakutangazia leo ukishafikia kiwango cha ukomavu, mbingu itafunguka kwa ajili yako.
Kusanyiko hili ni kusanyiko la wakomavu, na baada ya kusanyiko hili mbingu itazungumza juu yako.

Yeyote anayekushikilia, ajue kwamba wewe siyo mtoto tena unaweza kumiliki na kutawala.

Je, uko tayari kwa mambo makuu?
Huu ni wakati wako wa kupokea baraka kubwa.

MAJIRA YA MUNGU

Majira na nyakati zimewekwa na Mungu.
Mafanikio yako hayatokani na elimu, wala umri, bali utii wako kwa Mungu.

Haya ndiyo majira yako ya kuchukua nafasi yako na kumiliki.
Kama uko katika biashara, fahamu kuwa hakuna mkopo utakaoleta utajiri wa kweli;
Lakini Mungu wa Mbinguni kupitia utii wako, atakupa mafanikio ya kweli.

Ayubu 22:28 “Nawe utakusudia neno, nalo litathibitika kwako.”

Ninakutangazia leo, kwa sababu ya utii wako, madeni yako yanafutwa.
Utaishi maisha huru, bila madeni, na Mungu atakupa mtaji wako mwenyewe.

Kuna zaidi ya kinachotosha kwa ajili yako na hata kwa jirani zako!
Sababu pekee inayokufanya ushindwe kupokea ni kiwango cha haki ndani yako.
Nakutangazia sasa pokea zaidi ya ulichotarajia!

TANGAZO LA KIUNABII

Bonde ni ishara ya kiwango cha chini cha maisha.
Lakini leo, Bwana anakupandisha juu!

Kiwango chako cha kuishi kinaongezeka.
Nakataa maisha ya chini, na natangaza juu yako
Upako wa kuinuliwa ukakujilie!

Ukabadilishe nyika yako na kuwa bustani ya Edeni katika jina la Yesu.
Ninatangaza kuwa maisha yako ya giza yamekwisha sasa utaona nuru mpya.

Katika kusanyiko hili la mwaka 2025,
Bwana akakuinue katika viwango vipya vya baraka, mafanikio, na mamlaka ya kiroho.

HITIMISHO

Wapendwa, usiache imani yako moyoni pekee.
Cho chote unachoamini, kikiri kwa kinywa chako ndipo utakimiliki.

Huu ni wakati wa kanisa kusimama, wakati wa waamini kukua na kumiliki.
Bwana anasema:

“Simama katika nafasi yako, kwa maana nimekuita kwa ukuu.”

Amina.