Dawa Tatu Za Mungu: Imani, Tumaini Na Upendo

Mhubiri: Askofu Charles Kariuki – Kenya)

Siri kuu ya ushindi wa kila Mkristo. Mungu ana dawa tatu za kiroho ambazo anatupatia kila mmoja wetu kwa ajili ya maisha yetu ya kila siku. Dawa hizi si za hospitali, bali ni za uzima wa roho, nafsi na mwili.
Mungu anataka uzibebe, uzihifadhi moyoni na uzitumia mara tatu kwa siku bila kuruka hata moja.

Swali ni: Dawa hizo ni zipi?
1 Wakorintho 13:13“Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo.”

UFAFANUZI WA DAWA TATU ZA MUNGU

IMANI

Imani ni uwezo wa kuamini kile ambacho macho yako hayajioni.
Ni nguvu ya kumwamini Mungu hata kama mazingira yako yanaonyesha hali tofauti.
Waebrania 11:1 “Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana.”

Imani ndiyo inayoanzisha safari yako ya kiroho. Bila imani haiwezekani kumpendeza Mungu.

TUMAINI

Tumaini ni nguzo ya kusubiri ahadi za Mungu kwa uvumilivu na ujasiri.
Ni imani iliyo katika mchakato wa kutimizwa.
Warumi 5:5a “Na tumaini halitahayarishi.”

Hata kama mambo yako hayaendi kama ulivyopanga, usikate tamaa endelea kuwa na tumaini.
Tumaini ndilo lililomfanya Ibrahimu kuendelea kusubiri hata akiwa na umri wa miaka 99, bila mtoto, akiamini kuwa Mungu atafanya alivyosema.

UPENDO

Upendo ni dawa kuu kuliko zote.
Ni nguvu inayounganisha imani na tumaini zikafanya kazi.
1 Wakorintho 13:13 – “…na katika hayo lililo kuu ni upendo.”

Bila upendo, imani inakuwa baridi na tumaini linapoteza mwelekeo.
Upendo ni moyo wa Mungu. Ndiyo sababu Yesu alitoa uhai wake kwa ajili yetu kwa upendo.

MFANO WA IBRAHIMU

Mwanzo 18:19 – “Kwa maana nimemjua ya kwamba atawaamuru wanawe, na nyumba yake baada yake waishike njia ya Bwana…”

Ibrahimu alikuwa mfano bora wa kutumia dawa hizi tatu:

  • Alikuwa na imani kwa maneno ya Mungu.
  • Alikuwa na tumaini kwamba ahadi itatimia licha ya uzee wake.
  • Alikuwa na upendo kwa Mungu kiasi cha kumtoa mwanawe Isaka kama dhabihu.

Kwa sababu ya dawa hizi tatu, Mungu akamtimizia Ibrahimu ahadi zake – akawa baba wa mataifa mengi.

MAOMBI NA MATUMIZI YA DAWA TATU

Kama vile mgonjwa akipewa dawa na daktari anatakiwa kuzitumia mara tatu kwa siku, vivyo hivyo na wewe:

  • Asubuhi: tumia Imani – amka ukiamini Mungu ana mpango mzuri kwa siku yako.
  • Mchana: tumia Tumaini – ukikabiliwa na changamoto, jipe moyo, usikate tamaa.
  • Jioni: tumia Upendo – samehe, penda watu, fanya mema bila kuchoka.

Ukitumia dawa hizi kila siku, kamwe hautaibika, kwa maana tumaini halitahayarishi.

HITIMISHO

Mpendwa, changamoto zako zinaweza kuwa nyingi afya, kazi, elimu, ndoa, au biashara lakini Bwana anasema leo:
“Tumia dawa tatu za Mungu – Imani, Tumaini na Upendo.”

Hata ukizungukwa na maadui elfu kumi, hautaogopa; ukiwa na Imani, Tumaini na Upendo, hautashindwa.
Mungu ni mwaminifu. Yeye hachoki, hadharauliwi, hapungukiwi, wala haumwi.
Alichokuahidi, atakutimizia!