Ibada ya Jumapili 21/09/2025

SOMO: KUTENDA, KUONGEA NA KUFIKIRI KWA KUFUATA MAFUNDISHO YA MUNGU

Mchungaji Aimana Dominick – Kanisa la Efatha Mwenge

Yohana 20:22 “Akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu.”

Wapendwa, kipimo ambacho umemgeukia Mungu ndicho kipimo ambacho atamimina nguvu Zake na furaha Yake ndani ya maisha yako. Hivyo basi, fanya uamuzi wa kumgeukia Mungu kwa asilimia mia moja ili upokee furaha Yake kamili.

Mbinguni kumeingiza majira mapya, majira ya kiungu. Katika majira haya mapya, mbingu inatarajia kuona mambo mapya katika maneno yako, katika matendo yako, na katika mawazo yako.

Mbingu inatarajia kuwa maneno yako, matendo yako, na mawazo yako yaendane na mafundisho ya Mungu ambayo umeyapokea. Hakuna wakati ambapo mbingu imetupa mafundisho ambayo hayawezi kuishiwa. Mbingu haitarajii tusiseme, “Hili siwezi kufanya,” kwa maana tunaweza kufanya mambo yote katika Kristo atutiaye nguvu. Unapotenda kwa kufuata mafundisho ya Mungu, unaiweka mbingu kufanya kazi kwa niaba yako.

Unapofanya mbingu iamini kuwa kweli unaamini hakuna lisilowezekana, ndipo unatoa nafasi kwa mbingu kuendelea kufanya kazi katika maisha yako. Hivyo basi, ikiwa unataka kupokea uponyaji wa kiungu katika eneo lolote la maisha yako, ni lazima usamehe kama Mungu anavyosamehe.

Shetani hujaribu kutujaza uchungu, lakini Mungu ametupa Roho Mtakatifu ili atuwezeshe kusamehe. Roho Mtakatifu hutupa nguvu ya kuachilia majeraha na maumivu ambayo tukiyashikilia, hufungua mlango wa magonjwa yasiyotibika. Ndiyo maana tunahitaji msaada wa kiungu ili tupate kuonja uponyaji wa kiungu.

Zaburi 103:3 “Akusamehe maovu yako yote, Akuponya magonjwa yako yote.”

MAOMBI

Ee Baba wa Mbinguni, kwa unyenyekevu ninakuja mbele zako nikiomba unijaze kwa Roho wako Mtakatifu.

  1. a) Natamani kutiwa nguvu na kuhamasishwa na Roho Mtakatifu ili niweze kushinda kila maumivu.
    b) Nakushukuru, Ee Baba wa Mbinguni, kwa uwepo wa Roho Mtakatifu moyoni mwangu na katika maisha yangu ya kila siku.

Ee Baba wa Mbinguni, niko tayari kuhamasishwa na kuongozwa na Roho Mtakatifu.
Kuanzia siku ya leo, Ee Baba wa Mbinguni, nielekezwe na Roho Mtakatifu ili nitembee katika msamaha wako.