Ibada ya Jumapili 28/09/2025

MAMBO YANAYOONDOA FURAHA YA WOKOVU

Mtume na Kiongozi wa Kiroho – Noel Kapinga

Wapendwa, furaha ya wokovu ni zawadi kutoka kwa Mungu. Ni ile amani ya ndani, furaha ya kiungu, inayotutia nguvu kutembea kwa ujasiri mbele za Muumba wetu. Lakini yapo mambo ambayo yanaweza kusababisha furaha hii kufifia moyoni mwa muumini.

Kwanza, dhambi huiba furaha. Mwanamume au mwanamke anapotenda dhambi mbele za Mungu, ujasiri mbele ya kiti cha neema hupotea. Dhambi hututenga na Mungu, na ushirika unapovunjika, furaha huondoka.

Pili, moyo ulioumia hupoteza furaha. Mithali 4:23 “Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo, Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima”. inatukumbusha tulinde mioyo yetu kwa bidii zote, kwa maana kutoka humo hutoka chemchemi za uzima. Moyo uliojaa maumivu, uchungu, au vidonda visivyoponywa hauwezi kushikilia furaha ya wokovu.

Tatu, furaha hupotea kwa kusikiliza ovyo tunapofungua masikio yetu kwa sauti zisizofaa, ushawishi usiomcha Mungu, au mafundisho yasiyojenga, furaha ya kiroho huanza kuyeyuka.

Nne, matarajio yanapochelewa hutunyong’onyesha. Maandiko yanasema katika Mithali 3:30, “Usimshitaki mtu bure, ikiwa hakukutendea mabaya.” Tumaini linapochelewa, kukata tamaa hutokea, na tusipokuwa waangalifu, furaha hubadilishwa na uzito wa moyo.

Tano, roho ya uzito katika maamuzi inaweza kuizima furaha. Moyo unapoelemewa na kujaa wasiwasi, furaha haiwezi kutiririka kwa uhuru.

DALILI ZA KUHESABU KUWA UMEPOTEZA FURAHA YA WOKOVU

Ni kwa namna gani unaweza kujua kama furaha ya wokovu haipo tena ndani yako?

Kwanza, unaanza kumtumikia Mungu kwa uzembe. Pale ambapo zamani ulitumikia kwa moto na uaminifu, sasa unafanya kwa kutojali, bila bidii, bila imani, bila kujitoa iwe katika uchungaji, huduma, au mwito wowote Mungu aliokupa.

Pili, unaanza kukumbatia uongo. Roho ya uongo huanza kutawala. Biblia inasema katika Isaya 28:15, “Tumefanya uongo kuwa kimbilio letu, na kwa hila tumejificha.” Ukweli unapoondoka maishani mwako, hiyo ni dalili kuwa furaha ya wokovu imepotea.

Tatu, kutakuwapo na kukosa shukrani. Badala ya kushukuru, unalalamika. Badala ya kuona wema wa Mungu, unaona kasoro za wengine pekee. Badala ya kuhesabu baraka, unaanza kuhesabu makosa ya watu waliokuzunguka. Hiyo wapendwa, ni ishara ya wazi kwamba furaha imepotea.

Furaha ya wokovu ni ya thamani kubwa. Ni mafuta yanayodumisha taa ya imani yetu iendelee kuwaka. Tuilinde, tuitunze, na tuenende kwa utiifu ili nuru ya Kristo isiwahi kufifia ndani yetu.