MTUME NA NABII JOSEPHAT ELIAS MWINGIRA

1. Nguvu ya Msalaba

1 Wakorintho 1:18
“Kwa maana neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu.”

Kwa wale wanaopotea, ujumbe wa msalaba ni upuzi, lakini kwa wale wanaookolewa ni nguvu ya Mungu. Lazima uelewe ni nani anayetafakari kuhusu wokovu mara kwa mara wale wanaotafakari kuhusu wokovu mara zote wanakua kiroho, kiakili, na hata kiuchumi. Lakini wale wanaopuuzia wokovu, hata kama wanadai wameokoka, maisha yao yanazidi kudidimia siku baada ya siku, na wanakumbwa na matatizo kwa sababu hawatafakari kuhusu wokovu.

Nguvu ya msalaba inakukumbusha jinsi ya kuishi. Lakini kwa wale wanaopotea, ujumbe wa msalaba hauna maana ndiyo maana Yesu alisema, “Mtu yeyote anayetaka kunifuata, na ajitwike msalaba wake anifuate.” Hii inamaanisha kila aliyeokoka ana msalaba wake wa kubeba. Yesu alikufa kwa ajili yako je, wewe unakufa kwa ajili ya nini? Swali ni, unakufaje? Kama umeokoka kweli au la, Yesu alisema, “Kama unanipenda, jitwike msalaba wako unifuate.”

Wakati wa Musa, wale nyoka walipowauma watu, Mungu alimwambia Musa asiwaombee kwa sababu kila mtu ana safari yake huwezi kuwaombea kila mtu; badala yake, Mungu alimweka Musa kama kiongozi wao. Kila mtu alipaswa kutembea kwa miguu yake mwenyewe, na ndiyo maana safari haikuwa rahisi. Mungu alimwagiza Musa atengeneze nyoka wa shaba lakini kwa nini shaba?

Usitazame kinachokuuma, bali tazama mbele na songa mbele. Hata katika Neno, wale waliokataa kuutazama ule nyoka wa shaba walikufa pale pale. Ndiyo maana Mungu baadaye alimtuma Yesu, ili yeyote atakayetazama msalaba atapokea nguvu ya Mungu ndani yake, mizigo yake itaondoka, na atakuwa huru.

Yesu aliwaambia wanafunzi wake, “Mtu yeyote anipendaye, na anifuate kwa kubeba msalaba wake.” Kubeba msalaba ni jambo gumu sana. Kama unataka kuelewa ugumu wake, soma Biblia Yesu alipochukua msalaba wake, Simoni alilazimika kumsaidia. Kwa nini? Kwa sababu Mungu ametutumia Msaidizi Roho Mtakatifu ili atusaidie kubeba misalaba yetu.

Nguvu ya msalaba inakusaidia kushinda yale mambo yanayokushinda. Unapoutazama msalaba, yale mambo yanayokuumiza yanaondoka. Usiondoe macho yako msalabani wengi wamepoteza msalaba wao, na maisha yao yamekuwa ya hovyo.

Ukipenda kubeba msalaba, lazima uvumilie maumivu bila kukimbia, maana uvumilivu unakupeleka mahali pa kushuhudia nguvu ya Mungu. Katika safari ya kubeba msalaba, vikwazo vitaibuka kukuzuia usifike mahali pa kufa kwa kila kitu ndani yako lakini lazima utembee na msalaba wako mpaka uufikie msalaba wa kusulubiwa.

Ukishasulubiwa, kila kitu ndani yako kinakufa pale, na unaanza kutembea kwa ujasiri. Wengine wametupa misalaba yao, wakarudi nyuma, na ukiwauliza wanasema, “Tumechoka.” Lakini lazima ukumbuke kubeba msalaba wako mpaka uufikie msalaba wa kusulubiwa.

2. Nguvu ya Msamaha

Wakolosai 1:13-14
“Naye alituokoa kutoka katika mamlaka ya giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi.”

Unapobeba msalaba wako na kufika mahali pa kusulubiwa, ndipo ukombozi huanza katika maisha yako. Ukombozi hauanzi pindi unapokiri kwa kinywa chako, kwa sababu ukombozi ni mchakato wa kila siku lakini toba hutokea mara moja.

Unampokea Yesu na wokovu. Ndiyo maana Biblia inasema, “Mtaijua kweli, nayo kweli itawaweka huru.” Kadri unavyoijua kweli, ndivyo unavyokuwa huru zaidi. Kumuijua kweli kunaleta msamaha na kunabadilisha maisha yako unatoa maisha yako kwa Mungu.

Ni lini unasema umeutoa maisha yako kwa Kristo? Ni pale unapoweza kusema kwa ujasiri, “Maisha yangu ni ya Kristo.” Kubeba msalaba kunaleta msamaha, ambao unakuhamisha kutoka hali moja kwenda nyingine.

Zaburi 103:3
“Akusamehe maovu yako yote, Akuponya magonjwa yako yote.”

Msamaha unabeba uponyaji. Utaona nguvu ya msamaha unapoendelea kubeba msalaba wako — Mungu ana uwezo wa kukusamehe, na unapopokea msamaha, unahitimu kuwa mtu wa uponyaji. Kwa hiyo, msamaha ni muhimu sana.

3. Siyo Kila Mtu Anahitaji Ukombozi Wengine Wanahitaji Msamaha

Ufunuo 5:9-10
“Nao wakaimba wimbo mpya wakisema: Wastahili wewe kuutwaa ule gombo, na kuzifungua muhuri zake, kwa maana ulichinjwa, ukamnunulia Mungu kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa, ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi.”

Ukiwa na ufahamu huu, unabeba nguvu ya msamaha na ukombozi. Lazima ujue kuwa umenunuliwa kwa damu ya Yesu. Ingawa mababu zako waliweza kukuzaa au kukuuza katika utawala wa giza, Yesu alikununua kwa damu yake.

Waefeso 1:7
“Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake.”

Umenunuliwa na damu ya Yesu.

Wengine wanahitaji nguvu ya uponyaji kwa sababu wamebeba majeraha. Wanahitaji uponyaji kwa sababu kiakili na kihisia wameumizwa sana. Labda wakati wa malezi yako, kuna jambo lilitokea na kila ukilikumbuka, machozi yanatoka hilo ni jeraha. Inaweza kuwa katika ndoa yako au katika maisha mengine, na unapoikumbuka hali hiyo, unahisi huzuni au kukataliwa.

1 Petro 2:24
“Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, ili tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na kwa kupigwa kwake mliponywa.”

Huwezi kwenda mbali ikiwa hujapokea uponyaji kutoka mambo ya kale yaliyokuumiza. Unaweza kuomba mambo mengi kwa Mungu, lakini Yeye anaona vidonda vyako havijapona, na havimruhusu kutenda.

Watu wengi wamebeba majeraha ya utotoni, na majeraha hayo yanafuatana nao hadi kwenye ndoa wanaamini wanaume wote au wanawake wote ni sawa, kwa sababu ya yaliyowapata zamani. Lazima ujue watu ni tofauti ndoa ya mtu mwingine haiwezi kufanana na yako. Simama katika nafasi yako na utaona mabadiliko kwenye ndoa yako.

Zaburi 147:3
“Huwaponya waliovunjika moyo, na kuziganga jeraha zao.”