Kusimama Katika Nafasi Zetu

Mhubiri: Mtume na Nabii Josephat Elias Mwingira

UTANGULIZI

Wapendwa katika Bwana, leo tunajifunza kuhusu kusimama katika nafasi zetu tulizopewa na Mungu.
Kila mwanadamu ameumbwa akiwa na nafasi yake maalum mbele za Mungu, lakini nafasi hizo zimegawanyika katika hatua tatu kuu:

  1. Nafasi kabla ya dhambi
  2. Nafasi baada ya dhambi
  3. Nafasi baada ya wokovu

1: NAFASI KABLA YA DHAMBI

Kabala ya kuanguka kwa Adamu, mwanadamu aliishi katika bustani ya Edeni, akiwa katika utimilifu wa amri ya Mungu.
Mungu aliwabariki Adamu na Hawa, na akawapa maagizo matatu makuu:

Mwanzo 1:28

“Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi.”

Maagizo hayo yalikuwa:

  • Kuzaa, kuongezeka, na kuijaza nchi.
  • Kutiisha na kutawala.
  • Kulima na kutunza ardhi.

Haya yalikuwa maeneo matatu ya baraka, na mpaka leo hii, ndiyo lengo kuu la mwanadamu duniani.
Lakini baada ya dhambi, hali ilibadilika…

2: NAFASI BAADA YA DHAMBI

Baada ya dhambi, mwanadamu alipoteza ule utimilifu wa awali na akaanza kuishi katika huruma za Mungu.
Mtu akawa na aibu, akajitenga na uwepo wa Mungu, na kuhitaji msaada wa kiungu.

Kabla ya dhambi, mwanadamu aliishi kwa amri tatu rahisi:

  • Nafsi
  • Roho
  • Mwili

Lakini baada ya dhambi, maisha yakawa magumu kwa sababu mawazo ya mwanadamu yakawa maovu.

Mwanzo 6:5

“Bwana akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu sikuzote.”

Hivyo, mwanadamu alianza kuhitaji kanuni nyingi ili arudi katika mapenzi ya Mungu.
Uovu ukawa mwingi, na mwanadamu akahitaji wokovu wa kweli.

3: KUSIMAMA KATIKA NAFASI YA WOKOVU

Wokovu, wapendwa, unaanza kwa ukiri.
Bila ukiri, Mungu hawezi kufungua mambo yake kwako.
Kwa ukiri, unafunguliwa kuona mapenzi ya Mungu juu ya maisha yako.

Kabla ya dhambi, mwanadamu aliishi kwa amri ya upendo, upendo uliokuwa chini ya baraka.
Baada ya dhambi, mwanadamu aliishi kwa huruma za Mungu.
Lakini baada ya wokovu, tunaishi katika pendo la Mungu.

Warumi 10:9

“Kwa maana ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka.”

Kupitia ukiri, tunapata mambo mawili makuu:

  1. Haki ya Mungu
  2. Wokovu wa Yesu Kristo, ambao ni pendo la Mungu.

Unapokuwa na haki ya Mungu kwa imani, na wokovu kwa ukiri, unaanza kuishi kama mwana wa Mungu halisi.
Ukiri wako unakuhamisha kutoka katika dhambi kwenda katika haki ya Mungu.

4: HAKI YA MUNGU

Kwa nini tunahitaji haki ya Mungu?
Kwa sababu katika pendo la Mungu, kuna haki na wokovu.

Zaburi 37:24

“Ajapojikwaa hataanguka chini, Bwana humshika mkono na kumtegemeza.”

Mtu mwenye haki ya Mungu anapata kukubalika mbele za Mungu na wanadamu.

HAKI YA MUNGU HUFANYA MAMBO HAYA:

  • Inakupa kufanya vitu kwa usahihi.
  • Inaleta hekima, uaminifu, na imani.
  • Ni nguvu ya kutenda kazi.
  • Inaleta kukubalika mbinguni na duniani.
  • Inahakikisha mafanikio ya kudumu.

Zaburi 37:25

“Nalikuwa kijana nami sasa ni mzee, lakini sijamwona mwenye haki ameachwa, wala mzao wake akiomba chakula.”

Daudi alijua siri hii: Mwenye haki huwa hajatelekezwa.
Haki ya Mungu ndiyo ufunguo wa maisha mema na yenye neema.

5: TUNAPOSIMAMA KATIKA NAFASI ZETU

Tunaposimama katika haki ya Mungu, tunapata:

  • Hekima
  • Maarifa
  • Furaha

Mhubiri 2:26

“Kwa sababu Mungu humpa yeye aliyemridhia hekima na maarifa na furaha; bali mkosaji humpa taabu, ili kukusanya na kututa, apate kumpa huyo ambaye Mungu amridhia.”

Hivyo basi, chagua haki, kwa sababu ndani yake kuna hekima, maarifa, na furaha – yote haya yamo katika kifurushi cha baraka ambacho Mungu alimpa mwanadamu tangu mwanzo.

HITIMISHO

Leo Bwana anatuambia: “Simama katika nafasi yako.”
Usiruhusu dhambi, hofu, au mashaka zikutoe katika nafasi yako ya haki, baraka, na pendo.
Wokovu wako unakurudisha kwenye nafasi yako ya awali – nafasi ya mamlaka, utawala, na uhusiano wa karibu na Mungu.

Simama katika nafasi yako ya haki.
Tembea katika pendo la Mungu.
Tenda kazi zako katika hekima na maarifa.

Na mwisho, utajionea mwenyewe kwamba:
Baraka, Haki, na Pendo la Mungu litakuwa sehemu ya maisha yako kila siku.

MAOMBI

Ee Baba wa mbinguni, tunakushukuru kwa neno lako leo. Tusaidie tusimame katika nafasi zetu za haki, tusitetereke katika majaribu, na tuwe waaminifu katika wokovu wetu. Tujaze hekima, maarifa, na furaha yako. Katika jina la Yesu Kristo, tunasali, Amina.