Mahubiri Ka Kuvuka Mwaka Mpya – 31/12/2025

KANISA LA EFATHA
MTUME NA NABII: JOSEPHAT ELIAS MWINGIRA

Jiangalie mwenyewe: je, kweli unastahili kuwa hapa leo? Je, wewe ni bora kuliko wale waliokufa? Inaniletea machozi kuona tunavuka mwaka mmoja kwenda mwingine tukiwa bado hai. Ninajiuliza kwa nini watoto wanazaliwa na kufa, ilhali wazazi walidhani wao ndiyo muda wao ulikuwa umefika.. wengine walikufa kwa risasi, wengine kwa kupewa sumu, wengine kwa ajali. Lakini mimi na wewe tuko hai. Mwambie Mungu asante kwa kuwa hai.

Ni mambo mangapi umepitia, lakini leo bado upo hai mwambie Mungu asante.
Mpendwa, yule aliyekuponya amekuponya, nawe hujui siku ya kuondoka kwako; acha kujivuna, ishi maisha ya shukrani mbele za Mungu.

 

MANENO MATATU MUHIMU KATIKA BIBLIA

Katika Biblia kuna maneno matatu unayoyahitaji. Maneno haya hayatajwi sana na watu waliokoka na wanaompenda Mungu kwa sababu hawayaelewi vizuri maana yake. Maneno haya matatu yanabeba utatu wa Mungu:

1. Yehova Yire

Maana yake ni Mungu ni Mpaji na Mtunzaji. Neno hili ni muhimu sana kwa sababu ndilo linalolinda na kudumisha uumbaji. Yehova Yire ni Mungu anayekupa nguvu, Mungu mkarimu. Ili uishi, ule na unywe, unahitaji neno hili: Yehova Yire.

2. Shalom

Neno hili limeandikwa mara 305 katika Biblia. Linamaanisha usiogope. Shalom maana yake ni amani ya Bwana iwe juu yako. Linakuhifadhi, linakuzingira na kukulinda. Tunaposema Shalom, tunamaanisha: usiogope, uwe salama na uwe mshindi.

3. Efatha

Hili ni neno ambalo unaweza kulipuuza kwa sababu lilinenwa mara moja tu, lakini ndani ya utatu huu neno hili limo. Maana yake ni funguka. Kila kitu kilichofungwa, kilichokandamiza au kukuzuia unapotamka Efatha, kimekwisha. Japokuwa sikulielewa kikamilifu uzuri wa neno hili, sikulichagua kwa makusudi, lakini lina nguvu ya ajabu sana.

Efatha maana yake ni funguka. Chochote kinachokushikilia lazima kivunjike leo. Kila kitu kilichofungwa ili usiingie au usivuke upande wa pili, chochote kilichowekwa kukuzuia usiende mbele natangaza katika uwepo wa Bwana lazima kivunjike leo. Lazima uvuke upande wa pili; lazima upite, haijalishi ni nani aliyekufunga. Kama kuna jambo jema lililowekwa kwa ajili ya hatima yako, utaingia sasa. Amini, na litakuwa lako.

 

KUAMINI MUNGU NA WATUMISHI WAKE

Unaweza kumwamini Mungu, lakini si rahisi kumwamini mtumishi wa Mungu. Kwa nini? Kwa sababu yeye ni mwanadamu kama wewe, hivyo unaanza kumchunguza na kuangalia udhaifu wake. Lakini elewa hili: Mungu hatumii mwili, anatumia Roho. Ndiyo maana Biblia inasema, “Si kwa nguvu wala kwa uwezo, bali kwa Roho wangu,” asema Bwana. Roho wa Mungu anaweza kufanya chochote. Mwanangu, leo ni siku yako.

 

MAFUTA YA FURAHA NA MAISHA YA HAKI

Zaburi 45:7 inasema:
“Umeipenda haki na kuichukia dhuluma; kwa hiyo Mungu, Mungu wako, amekupaka mafuta ya furaha kuliko wenzako.”

Ukitaka kuwa na furaha maishani:

  • Chukia dhuluma
  • Penda haki

Haki ni nini? Ni kweli ya Mungu. Penda kweli ya Mungu. Unapofanya hivyo, hata kama mtu amekukosea, usimkosee pendelea haki. Unapopenda haki, Mungu anakupaka mafuta. Mafuta haya hayapakiwi na mchungaji wako bali yanatoka kwa Bwana wa mabwana. Yanapomshukia mtu, maisha yake yanaanza kustawi, kwa sababu mafuta ya furaha humfanya mtu astawi. Mtu aliyeokoka, anayechukia dhuluma na kupenda haki, maisha yake yanaonyesha mabadiliko.

Mafuta ya furaha yanakuja pale unapoamua kuishi maisha yanayompendeza Mungu. Utastaajabu kuona Mungu anakunyanyua kutoka hatua moja kwenda nyingine.

Unajua Mungu amekubadilisha hata kama unaishi mazingira yale yale.

 

MAISHA YA KRISTO NDANI YAKO

Wagalatia 2:20 inasema:
“Nimesulibiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili ninao katika imani ya Mwana wa Mungu, aliyenipenda akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu.”

Ukitaka mafuta haya yafanye kazi kwako, mtu akikusengenya au kukutukana, usikasirike hurumia. Hata Kristo alipokuwa akisulubiwa, alitangaza rehema.

Maisha ya wokovu ni maisha ya Kristo ndani yako. Si maisha yako tena, kama vile mke aliyeolewa hawezi kufanya maamuzi bila kumshirikisha mume wake. Kuna siri kubwa unapokuwa mwenye haki wa Mungu: lazima ufike mahali useme, “Si mimi ninayeishi, bali Kristo anaishi ndani yangu.” Maisha ya mtu anayekwenda mbinguni ni maisha ya kuishi kana kwamba Kristo mwenyewe ndiye anaishi. Lazima utangaze kuwa wewe ni wa Kristo.

Ukiona mtu mwingine ameanguka dhambini, usibebe siri yake na kuisambaza. Mungu alikuruhusu uione, lakini wewe si mjumbe wa habari mbaya. Uliipeleka wapi siri uliyoiwona? Kama unataka kuwa msiri wa Mungu, kataa kubeba na kusambaza makosa ya wengine.

 

KULA MEMA YA NCHI: SIRI YA KUTII

Isaya 1:18–19 inasema:
“Haya, njoni tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji… Kama mkikubali na kutii, mtakula mema ya nchi.”

Wewe uliyeokoka ni wa Mungu, na maisha yako ni ya Mungu. Hivyo unapaswa kula mema uliyoandaliwa, lakini kuna mambo lazima uyaache ili ule.

Biblia inasema, “Kama mkikubali na kutii, mtakula mema ya nchi.” Ili ule mema ya nchi, Mungu kwanza anaondoa uovu unaokuzuia kupokea. Kama umetii, je, unakula mema ya nchi? Kama hauli, jua bado hujakubali na kutii kikamilifu.

Kutii ni nini? Ni kufanya kile ambacho hupendi lakini kinapaswa kufanywa. Unapofanya hivyo, Mungu anaondoa uovu ndani yetu, anaondoa mifumo ya dhambi ya kurithi, kisha anarudisha mema yake, kwa sababu Mungu haweki mema yake mahali palipo na uovu.

Ukitaka kula mema ya nchi, elewa haya:

  1. Kiwango chako cha kukubali kinaamua ni kiasi gani cha dhambi, uovu na ubaya vitaondolewa.
  2. Kiwango chako cha utii kitaleta kiwango sawa cha kula mema ya nchi. Utii mkubwa baraka kubwa; utii mdogo mema machache. Kama utii wako ni kunena kwa lugha tu, unaweza kupata afya njema pekee.

Unapokubali kufanya kile ulichokuwa hukitaki, Mungu atafanya kile kilichokuwa kinakugomea kikutii. Hakuna kitu kinachogoma kama mafanikio, ndiyo maana waliofanikiwa ni wachache.

Tambua kile kinachokugomea, kiandike, kisha muombe Mungu akuonyeshe ni wapi hujatii ili vitu hivyo vianze kukutii.

Je, uko tayari kutii? Kama uko tayari, Mungu akujalie kula mema ya nchi.

 

MWAKA WA KUFANYA MAPENZI YA MUNGU

HUU NI MWAKA WETU WA KUFANYA MAPENZI YA MUNGU ILI ATUBARIKI.

Mwaka 2025 Mungu alituambia tusimame kwenye nafasi zetu kwa sababu tunakaribia urithi wetu. Mungu anatuelekeza kwenye wema wake; haya yote ni maandalizi ya kutufikisha kwenye uzuri wa utukufu wake. Mungu anataka nini kwetu? Anataka mwaka huu tufanye mapenzi yake. Huu ni mwaka wa kufanya mapenzi ya Mungu. Ninaamini kwa moyo wangu wote kuwa kwa sababu huu ni mwaka wa kufanya mapenzi yake, kuna watu watakuwa si wa kawaida nami ni mmoja wao.

Nini kitatokea? Wengine watapokea karipio kama hawataki kutii, kwa maana Biblia inasema, “Wale niwapendao nawakemea.” Huu ni msimu wa kufanya mapenzi ya Mungu, kwa maana Mungu ameruhusu tule na tunywe.

Waefeso 5:17:
“Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu mapenzi ya Bwana ni nini.”

Safari hii sisi si wajinga. Mungu anaweza kumwagiza mtu aliyeko Ujerumani akuletee pesa za biashara; anaweza kumwambia jirani yako akusaidie. Lakini swali ni: Mungu anapendezwa kwa kiwango gani na maisha yako?

Nenda ukale mema ya nchi.

 

NENO KWA YOSHUA

Mungu alimwambia Yoshua (Yoshua 1:7):
“Uwe hodari na shujaa sana, uangalie kutenda sawasawa na sheria yote… ndipo utakapofanikiwa sana kila uendako.”

Mwanangu, fanya yale ninayokuambia; usitafute njia zako. Ukiwa chini ya mtumishi wa Mungu, na ukitamka maneno aliyoyatamka kwa usahihi, yanakuwa yako, na dunia lazima itii.

Umeelewa nini? Umeambiwa nini?

Tena Zaburi 45:7 inasema umepewa mafuta ya furaha. Mafuta haya yatatiririka kwako unapokubali na kutii hata yale mambo unayoona yana aibu kuyafanya. Unapofanya hivyo, Mungu atafanya yale unayotaka yakutii.

Mafuta yatatiririka, na Mungu ataondoa kila ugumu na uovu ili ule mema ya nchi. Mwaka 2023 alisema tutamiliki; mwaka jana alisema tukae kwenye nafasi zetu. Sasa mwaka huu anaamuru tutimize mapenzi yake ili atubariki.

Mwana wa Mungu, mwaka huu 2026, kubali na utii ili upate kubarikiwa.

 

MAOMBI

  1. Muombe Mungu akupe neema ya kufanya yale atakayokuambia (uwe mtii).
  2. Bwana, nijaalie kufanya mapenzi yako na yale yakupendezayo.

 

UKIRI

  • Ee Bwana, moyo wangu, njia zangu na kazi zangu zikufurahishe; maneno yangu yakupendeze; macho yangu yakutazame wewe pekee.
  • Bwana, leo ninaanza siku na mwaka mpya; nataka kila kitu kiwe kipya. Roho za magonjwa hazina nafasi ndani yangu; magonjwa, udhaifu, ajali, habari mbaya, vifo na majanga havina nafasi kwangu. Navifungia nje, maana mimi ni mteule wa Bwana.

 

TAMKO (AMRI)

  • Kwa jina la Yesu, naamuru mifupa yangu iwe sawa na yenye nguvu ili niishi muda mrefu; kila kiungo kikae mahali pake bila kuteguka wala kuvunjika hadi siku ya kuondoka duniani.
  • Bwana Yesu, naamuru viungo vyangu vyote mapafu, figo, ini, viungo vya uzazi, kongosho na vyote viwe salama. Kila kinachoingia mwilini mwangu kiwe cha kuurutubisha; kila ugonjwa uondoke kwa jina la Yesu.
  • Kila mlango uliofungwa kwangu, natangaza Efatha kwa jina la Yesu.
  • Kuanzia leo, kila silaha iliyoundwa dhidi yangu naihukumu kwa jina la Yesu; kila kikao cha adui dhidi yangu navivunja, washindwe na wasionekane tena.
  • Bwana Yesu, napinga kila kinachokula fedha zangu.
  • Bwana, kwa mamlaka ya jina la Yesu, nakata nguvu za kila kundi linaloinuka kinyume changu.
  • Kila mpango nilioufanya au nitakaoufanya wa kuingiza kipato ufanikiwe kwa jina la Yesu, wala hakuna kitakachozuia.