Mhubiri: Askofu Charles Kariuki Kenya
UTANGULIZI
Inawezekana kuna mambo yaliyotokea kwa ajili yako ambayo si mazuri katika siku hii, lakini mimi kama balozi wa mbinguni ninakutangazia kwamba ijumaa hii utaifurahia.
Ijumaa yako imebarikiwa utaifurahia na utamshukuru Mungu kwa ajili ya siku hii.
UKIRI
“Baba katika jina la Yesu, ninakubaliana na Neno lako kwamba ijumaa yangu imejawa na furaha, imejawa na wema, na si vinginevyo. Kwa jina la Yesu, naibariki ijumaa yangu na ninaianza kwa tumaini kubwa, nami najua tumaini langu halitazimishwa.”
MTAZAMO
Ikiwa umeshawekwa katika nafasi yako katika Ufalme wa Mungu na umeitambua nafasi hiyo, kinachofuata ni kudumu katika hiyo nafasi.
Na kudumu kunahitaji mtazamo sahihi kumtazama Yesu pekee.
Waebrania 12:2
“Tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba, na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu.”
USITULIE ENDELEA KUPANDA
Usitulie baada ya kufanikiwa mara moja; nyuma ya mlima kuna milima mingine.
Mshukuru Mungu kwa mafanikio ya jana, lakini jiandae kwa yale mapya ya mbele yako.
Mithali 4:25
“Macho yako yatazame mbele, na kope zako zitazame mbele yako sawasawa.”
Biblia inaposema macho yako yatazame mbele, haizungumzii macho ya mwilini, bali macho ya moyo wako mtazamo wako wa ndani.
Nguvu ya kusonga mbele ipo katika mtazamo wako.
Ukielekeza macho yako kwa Yesu, utapata moyo wa kuendelea.
MFANO WA WAKOMA WANE
2 Wafalme 7:3-8
Wakoma wanne waliokuwa nje ya mji wa Samaria walijiuliza:
“Kwa nini tukae hapa hata tufe?”
Walibadilisha mtazamo wao wakaona uwezekano wa kuishi badala ya kufa.
Waliinuka na kwenda, na Mungu akatembea nao.
Mwana wa Mungu, badilisha mtazamo wako kutoka kifo kwenda uhai, kutoka kukata tamaa kwenda tumaini.
Ukimtazama Yesu, utapata nguvu ya kuinuka na kufikia yale Mungu aliyokusudia.
USIANGALIE NYUMA
Wafilipi 3:13–14
“Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu: nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele, nakaza mwendo niifikie tuzo ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu.”
Mtume Paulo alisonga mbele kwa sababu ya mtazamo wake.
Haikuwa tu kwa sababu ya upako, bali kwa sababu aliweka macho yake kwa Yesu.
USIANGALIE MLIMA ANGALIA YESU
Usiangalie ukubwa wa tatizo lako.
Zaburi 121:1-2
“Nitaelekeza macho yangu milimani; msaada wangu watoka wapi?
Msaada wangu watoka kwa Bwana, aliyezifanya mbingu na nchi.”
Mlima wako ni mdogo ukimlinganisha na Yesu.
Ukimtazama Yesu, matatizo yako yatakuwa kama panzi mbele yako.
2 Wakorintho 4:18
“Tukiyaangalia yasiyoonekana; kwa maana yanayoonekana ni ya muda tu, bali yasiyoonekana ni ya milele.”
Adui anaweza kuwa mkubwa kama Goliathi, lakini Yesu ni mkuu kuliko Goliathi wako.
1 Samweli 17:45-47
Daudi akamwambia yule Mfilisti, “Wewe wanijia kwa upanga na mkuki na fumo, lakini mimi nakujia kwa jina la Bwana wa majeshi…”
KAZA MWENDO
Kati ya majaribu mengi, kaza mwendo.
Badili mtazamo wako kutoka kwenye matatizo na uweke kwa Yesu.
2 Wafalme 2:9-10
“Elisha alipomwomba Elia sehemu ya roho yake mara mbili, alitakiwa kutazama “Ukiniona nikienda, utapata.”
Elisha aliendelea kutazama mpaka akapokea kile alichokitamani.
HITIMISHO
Ushindi wako unategemea mtazamo wako.
Usiangalie maadui, matatizo au milima, bali mtazame Yesu.
Yohana 16:33
“Katika ulimwengu mna dhiki; lakini jipeni moyo, mimi nimeushinda ulimwengu.”
MAOMBI YA KUHITIMISHA
“Bwana Yesu, nisaidie kuweka macho yangu kwako.
Niondolee hofu na mtazamo hasi.
Nijaze tumaini jipya na nguvu za kusonga mbele.
Naomba unitie moyo kila siku ili nisitetemeke bali niwe imara katika imani yangu.
Asante kwa ushindi ulionipa.
Kwa jina la Yesu, Amina.”