Mungu Anabadilisha Hatima Yako

Mhubiri: Mchungaji James Commey (Kutoka Denmark)

MAANDIKO:

  • 2 Timotheo 3:16
  • Mwanzo 1:26
  • 1 Mambo ya Nyakati 4:9

UTANGULIZI:
Ahadi za Mungu ni Amina na Kweli. Mungu ametupa mtazamo wa kutatua matatizo yetu.
Nguvu ya kubadilisha mazingira yako inategemea ufahamu wako juu ya Neno la Mungu.
Kusudi la Neno la Mungu ni kuona, kurekebisha, na kutoa maagizo ili tufanye yaliyo sahihi.

Biblia inasema katika 2 Timotheo 3:16:
“Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki.”
Kwa hiyo, Neno la Mungu si hadithi tu bali ni mwongozo wa kuishi maisha sahihi na kutambua nafasi yetu katika Kristo.

  1. UFAHAMU WA MFANO WA MUNGU NDANI YAKO
    Mungu alituumba kwa mfano wake mwenyewe. Huo mfano lazima uongoze maisha yako.
    Wewe si mfano wa ibilisi, si mfano wa maovu, bali ni mfano wa Mungu mwenyewe, Muumbaji wa mbingu na nchi.
    Mtazamo huu wa kiungu ni lazima uingie akilini mwako ili ukae sawasawa na nafasi uliyopewa na Mungu.
    Usiishi chini ya utambulisho wa uongo. Jitambue kama mtoto wa Mungu aliyeumbwa kutawala na kumiliki.
  2. MPANGO WA MUNGU JUU YA MAISHA YAKO
    Mungu alipotuumba, alituumbia kwa kusudi maalum.
    Mwanzo 1:26 inasema:
    “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.”
    Mungu alitupa majira, majukumu, mamlaka, na utukufu.
    Hajakuokoa bila kusudi.
    Ametuvika utukufu na heshima, ametupa mamlaka juu ya vitu vyote, na ametuita kutawala.
    Kwa hiyo, chukua nafasi yako! Wewe ni mtawala wa Mungu duniani.
  3. HATIMA YAKO HAITEGEMEI JINA ULIPEWA NA WANADAMU
    1 Mambo ya Nyakati 4:9 inasema:
    “Naye Yabesi alikuwa mwenye heshima kuliko nduguze; na mamaye akamwita jina lake Yabesi, akisema, Ni kwa sababu nalimzaa kwa huzuni.”
    Wazazi wengi huwapa watoto majina kulingana na mazingira au matukio waliyopitia.
    Lakini Yabesi alikataa jina lililomfanya aishi katika huzuni.
    Jina au utambulisho uliotolewa na wanadamu hauamui hatima yako.

Labda uliitwa masikini, uliokataliwa, au usiyefaa lakini Mungu anakuita mkuu na mwenye heshima.
Namna watu wanavyokuita siyo namna Mungu anavyokuona.
Leo Mungu anabadilisha jina lako na kukurejesha kwenye hatima yako ya kweli.

  1. MUNGU ANABADILISHA NAMNA UNAVYOJIONA
    Gideoni alijiona mdogo na asiye na uwezo, lakini Mungu alimwita “shujaa.”
    Daudi alikataliwa na familia yake, lakini Mungu alimchagua kuwa mfalme wa Israeli.
    Hivyo pia wewe labda umekataliwa, umeonekana hauna maana, lakini Mungu anakwenda kukurejesha katika nafasi yako ya hatima.
    Wale waliokukataa wataanza kuona namna Mungu anavyokuona.
  2. KILA NENO HASI LITAVUNJIKA KWA JINA LA YESU
    Kila neno la kukatisha tamaa, kila utambulisho wa uongo, kila jina lililowekwa juu yako kinyume na kusudi la Mungu linafutwa leo kwa jina la Yesu!
    Mungu anakuinua juu ya huzuni, laana, na vizuizi vya zamani.
    Hatima yako iko mikononi mwa Mungu, si mikononi mwa wanadamu.

HITIMISHO:
Wewe ni mfano wa Mungu, umeumbwa kutawala, kumiliki, na kuleta utukufu wa Mungu duniani.
Usikubali jina, huzuni, au mazingira yakutenganishe na kusudi la Mungu.
Kama Yabesi, inuka, omba, na sema: “Ee Mungu, nibariki kweli kweli, panua mipaka yangu, na mkono wako uwe nami.”
Mungu anakurejesha leo katika nafasi yako ya utukufu na heshima.

MAOMBI:
Ee Mungu wa rehema, nisaidie kutambua nafasi yangu ndani yako.
Niondolee kila jina, kila neno, na kila laana isiyo kutoka kwako.
Nipe nguvu ya kusimama katika kusudi ulilonipa.
Badilisha jina langu, badilisha hatima yangu, na nielekeze katika njia ya utukufu wako.
Katika jina la Yesu Kristo, Amina.