MHUBIRI: Mchungaji Jens Garnfeldt (Kutoka Denmark)
MAANDIKO YA MSINGI:
Waefeso 1:3
“Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo.”
UTANGULIZI:
Biblia inatufundisha kwamba Mungu ametubariki ndani ya Kristo Yesu kwa baraka zote za kiroho katika ulimwengu wa roho.
Lakini mara nyingi, tumepunguza maana ya baraka tukidhani ni vitu vya kawaida kama kazi, gari, nyumba, au mke/mume.
Hata hivyo, mbaraka wa Mungu ni kitu kikubwa zaidi ya mali au vitu tunavyomiliki.
Mbaraka wa Mungu si kitu cha nje ni uwepo na uhalisia wa Mungu mwenyewe unaotiririka ndani ya maisha yetu.
Ni nguvu ya kiungu inayofanya mbingu na vitu vyote vitende kazi.
- MBARAKA WA MUNGU NI UWEPO WA MUNGU MWENYEWE
Biblia inasema Mungu ametubariki “kwa baraka zote za rohoni.”
Hii inamaanisha baraka si matokeo ya vitu bali ni Mungu mwenyewe akifanya kazi ndani ya maisha yako.
Kila kitu mbinguni kinasimama kwa nguvu ya mbaraka wa Mungu.
Mbaraka ni maisha ya kiungu yanayotiririka katika kila kiumbe kilicho mbinguni.
Ndiyo sababu Yesu alisema tuombe, “Mapenzi yako yatimizwe duniani kama huko mbinguni.”
Kwa nini? Kwa sababu kila kitu mbinguni kinaishi kwa mbaraka wa Mungu maisha ya kiungu, utakatifu, na nguvu.
- MBARAKA NI NGUVU YA KUFANIKIWA
Mungu anataka na wewe uishi katika mbaraka huo wa mbinguni hapa duniani.
Anataka maisha yako yawe na nguvu zake na utende kazi chini ya neema na ufanisi wake.
Mbaraka ni nguvu ya kiungu inayosababisha mafanikio.
Unaposema “nimebarikiwa,” inamaanisha maisha ya Mungu yanatembea ndani yako.
Mbaraka huu una uwezo wa kubadilisha mazingira yako, kufungua milango, na kuleta utukufu wa Mungu katika maisha yako.
- YESU ALICHUKUA LAANA ILI TUBARIKIWE
Wagalatia 3:13
“Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti.”
Yesu alibeba laana zote juu ya msalaba.
Kila laana iliyokuwa juu ya wanadamu ilichukuliwa na Yesu, ili sisi tuishi katika mbaraka wa Mungu.
Kwa hiyo, wewe haujalaaniwa tena umebarikiwa kwa baraka zote za kiungu ndani ya Kristo.
Usiishi chini ya hofu, huzuni, au laana za zamani.
Yesu alikomesha laana hiyo ili wewe utembee katika uzima na ufanisi wa kiungu.
- MBARAKA WA IBRAHIM UKO JUU YAKO
Mungu alimbariki Ibrahimu na kumfanya kuwa baraka kwa mataifa yote.
Kupitia Kristo Yesu, wewe pia umeshiriki mbaraka wa Ibrahimu.
Mbaraka wa Ibrahimu ni mbaraka wa:
- Kuongezeka
- Utajiri wa kiroho na kimwili
- Nguvu ya kushinda
- Kufanikiwa katika yote unayofanya
Biblia inasema: “Wewe umebarikiwa mara mbili!”
Hii ina maana kwamba hakuna upungufu tena katika maisha yako.
Baraka za Ibrahimu zimewekwa juu yako wewe ni mrithi wa baraka za mbinguni.
- MBARAKA NDIO CHANZO CHA MAISHA YA KIUNGU
Kila kitu kinachofanya mbingu itende kazi kiko ndani yako.
Roho wa Mungu anakaa ndani yako, na huo ndio mbaraka mkuu kuliko yote.
Ufalme wa Mungu uko ndani yako, na huo ufalme una nguvu ya kuleta mabadiliko katika dunia yako.
HITIMISHO:
Wewe umebarikiwa katika Kristo Yesu.
Mbaraka wako si matokeo ya vitu ni maisha ya Mungu ndani yako.
Umewekwa huru kutoka kwenye laana, umeingizwa katika baraka ya Ibrahimu.
Tembea kwa imani, jua kwamba mbaraka wa Mungu unakufuatilia kila siku ya maisha yako.
Kila unachogusa kibarikiwe, kila unachofanya kifanikiwe, na kila unapokwenda utukufu wa Mungu uonekane juu yako.
MAOMBI:
Ee Baba wa mbinguni, nakushukuru kwa kunibariki kwa baraka zote za kiroho ndani ya Kristo Yesu.
Ninakataa laana zote za zamani na ninapokea mbaraka wa Ibrahimu juu ya maisha yangu.
Nijaze nguvu zako, utukufu wako, na ufanisi wako.
Nitembee katika maisha ya kiungu kila siku, kwa jina la Yesu Kristo, Amina!