Somo: Utawala wa Mungu na Mamlaka ya Mtu

Mhubiri: Pastor Jens Garnfeldt (Kutoka Denmark)
Maandiko: Mwanzo 1:26, Zaburi 8:4 6, Zaburi 115:16

UTANGULIZI:
Biblia inasema katika Mwanzo 1:26, “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.”
Hapo tunaona kusudi kuu la Mungu kwa mwanadamu utawala. Mungu alimuumba mwanadamu si kwa bahati mbaya, bali kwa kusudi maalum la kutawala, kumiliki, na kuwakilisha mamlaka ya Mungu hapa duniani.

  1. MUNGU ALIMPA MWANADAMU UTAWALA
    Baada ya Mungu kuumba mbingu na nchi, alimuumba mwanadamu ili awe wakili wake duniani. Mungu alimpa nguvu, mamlaka, na baraka. Alisema, “Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitawala.”
    Adamu alikuwa mtawala wa dunia hii. Kila kitu kilitiishwa chini yake. Mungu alimvika taji ya utukufu na heshima kama Zaburi 8:4 6 inavyosema, “Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu; umemvika taji ya utukufu na heshima; umemtawaza juu ya kazi za mikono yako.”

Mwanadamu aliumbwa mdogo chini ya Mungu, lakini mkubwa kuliko viumbe vyote.
Hii inamaanisha kwamba wewe ni mwakilishi wa Mungu duniani, uliumbwa kwa sura na mfano wake.

  1. MUNGU ALIMPA MWANADAMU UMILIKI
    Zaburi 115:16 inasema, “Mbingu ni mbingu za Bwana, bali nchi amewapa wanadamu.”
    Hili si pendekezo; ni sheria ya ki-Mungu. Mungu aliamua kumpa mwanadamu mamlaka juu ya nchi. Hivyo, hakuna kitu kinachoweza kufanya chochote duniani bila ruhusa ya mwanadamu.
    Hata ibilisi mwenyewe hawezi kufanya lolote bila kupitia mwanadamu. Ndiyo maana Yesu ilimbidi azaliwe kama mwanadamu, ili kwa njia halali aweze kurejesha mamlaka iliyopotea.
  2. JINSI IBILISI ALIVYOCHUKUA MAMLAKA NA JINSI YESU ALIVYOREJESHA
    Ibilisi alimdanganya Adamu, na kwa dhambi hiyo, Adamu alipoteza mamlaka yake. Ibilisi akawa na ushawishi juu ya dunia. Ndiyo maana alimwambia Yesu, “Nitakupa milki yote ya dunia hii ukiniinamie.”
    Lakini Yesu hakuinama! Badala yake, alikuja kuchukua tena mamlaka hiyo kwa niaba ya mwanadamu.
    Yesu alifanyika dhambi ili sisi tuwe wenye haki. Alibeba laana ili sisi tuwe baraka. Alishuka hadi kuzimu, akamvua ibilisi mamlaka yote, na akatupa tena sisi wanadamu utawala na umiliki wa dunia hii.

Leo, mamlaka yako yamerudishwa. Uko huru! Umevikwa taji ya utukufu na heshima.
Jitambue! Wewe ni mtawala duniani kwa jina la Yesu Kristo.

  1. MUNGU ANATUMIA WANADAMU KUFANYA KAZI ZAKE DUNIANI
    Kila mtembeo wa Mungu duniani unahitaji mwanadamu. Mungu hatendi chochote duniani bila chombo chake.
    Unapolilia uamsho, Mungu humuinua mtu kama msaada. Katika taifa letu, Mungu amemuinua Mtume na Nabii Josephat Elias Mwingira kuwa chombo cha uamsho na mtembeo wa Mungu.
    Wakati taifa linapolilia mabadiliko, Mungu anajibu kwa kuinua mwanadamu.

Wewe unaweza kuwa chombo hicho!
Tamani kuwa mtu ambaye Mungu atatumia. Tamani kubeba uamsho wa kizazi hiki.

UNABII:
Tanzania itaingia katika uamsho wa kitaifa, na uamsho huo utatembea kote Afrika.
Ni wakati wa mtembeo mkubwa wa Mungu Tanzania.
Mungu anatembea na anatafuta vyombo vitakavyobeba moto wa utukufu wake.
Je, utakuwa mmoja wao?

Amina!