Ibada Ya Jumapili – 29.06.2025

NGUVU YA MSALABA NA MSAMAHA

Na Mtume na Nabii Josephat Elias Mwingira

  1. Nguvu ya Msalaba

1Wakorintho 1:18
“Kwa maana neno la msalaba kwao waliopotea ni upuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu.”

Halleluya!
Wapendwa, Biblia inasema neno la msalaba kwa waliopotea ni upuzi! Lakini kwetu sisi tunaookolewa ni nini? Ni nguvu ya Mungu!
Wacha nikuambie, wokovu ni safari, sio hadithi. Wale wanaoutafakari wokovu siku zote, wanaona ukuaji kiroho, wanaona ukuaji kiakili, na hata kiuchumi. Lakini wale wanaopuuza wokovu, hata kama wanajitangaza wameokoka maisha yao yanadidimia siku baada ya siku.

Yesu alisema, “Mtu akitaka kunifuata ajitwike msalaba wake anifuate.”
Kila mmoja wetu ana msalaba wake. Swali kwako leo Yesu alikufa kwa ajili yako, wewe unakufia nini? Je, kweli unakufa na dhambi zako, tamaa zako, kiburi chako? Au umeacha msalaba wako njiani?

Katika siku za Musa, watu walipoumwa na nyoka, Mungu hakumwambia Musa awaombee wote. Hapana! Kila mtu alipaswa kuutazama nyoka wa shaba. Ukikataa kutazama, ulikufa papo hapo! Vivyo hivyo leo ukikataa kuutazama msalaba wa Yesu, unakufa kiroho.

Msalaba ni maisha. Msalaba ni nguvu. Ukibeba msalaba wako, lazima uvumilie. Ndiyo maana Yesu alibebeshwa na Simoni. Hiyo ni ishara kwamba hatubebi wenyewe Roho Mtakatifu ndiye msaidizi wetu.

Wapendwa, nguvu ya msalaba itakuondolea mzigo wote. Itavunja minyororo ya dhambi. Lakini sharti usiache macho yako msalabani. Wengi leo wametoa macho yao msalabani, wakarudi nyuma maisha yao yamejaa vurugu. Lakini leo nasema: Rudisha macho yako msalabani, utapata nguvu ya Mungu!

  1. Nguvu ya Msamaha

Wakolosai 1:13-14
“Kwa maana alituokoa kutoka katika ufalme wa giza, akatuhamisha katika ufalme wa Mwanawe mpendwa, ambaye ndani yake tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi.”

Eeh, msamaha!
Wapendwa, unapoamua kubeba msalaba wako hadi pale pa kusulubiwa, hapo ndipo ukombozi unapoanza. Toba ni tendo la wakati mmoja, lakini ukombozi ni safari ya kila siku.

Biblia inasema, “Nanyi mtaijua kweli, nayo kweli itawaweka huru.” Kadri unavyojua kweli, ndivyo unavyokuwa huru zaidi. Ukimpa Kristo maisha yako, msamaha unakufuata, na unapopata msamaha, unapata na uponyaji!

Zaburi 103:3 inasema: “Anayesamehe maovu yako yote, anayeponea magonjwa yako yote.”
Halleluya! Msamaha na uponyaji havitengwi. Wapo hapa leo, mmebeba magonjwa siyo kwa sababu madaktari hawana dawa, bali kwa sababu hujapata msamaha wa kweli.

  1. Sio Kila Mtu Anahitaji Ukombozi, Wengine Wanahitaji Msamaha

Ufunuo 5:9-10 inasema:
“Kwa damu yako umewanunulia Mungu watu wa kila kabila, na lugha, na jamaa, na taifa.”

Damu ya Yesu imenunua watu wote. Lakini bado, wengine wameshikwa na majeraha ya ndani. Wapo hapa leo, majeraha ya utoto yamewabeba, majeraha ya ndoa, majeraha ya kuachwa, kukataliwa. Wengine kila wanapokumbuka yaliyopita, machozi yanatoka. Hayo ndiyo majeraha yanayozuia mkono wa Mungu kugusa maisha yako.

Lakini Biblia inasema:

1Petro 2:24
“Kwa kupigwa kwake, mliponywa.”

Zaburi 147:3
“Awaponya walio na moyo uliovunjika, na kuufunga vidonda vyao.”

Yesu ni mponyaji wa mioyo iliyovunjika. Leo nakutangazia kama umebeba majeraha ya zamani, damu ya Yesu inakufungua! Ukimpa Yesu nafasi, anakufunga vidonda vyako na anakupa mwanzo mpya.

Hitimisho:
Nguvu ya msalaba ndiyo msingi wa wokovu. Msamaha ni mlango wa uponyaji. Ukombozi ni safari ya kila siku. Wapendwa, tusibaki nyuma  tusijichoshe bali tusonge mbele tukibeba misalaba yetu, tukimtazama Yesu, aliye mwanzilishi na mkamilishaji wa imani yetu.