MHUBIRI: Askofu Thabo Masema, Afrika Kusini
Lazima uelewe kwamba ili huduma iwe na ufanisi, ni lazima kuwe na umoja kufanya kazi pamoja katika huduma. Ili kanisa liweze kukua na kuwa na nguvu, ni lazima liwe na umoja, kwa maana huko ndiko nguvu yake ilipo.
Kuna watu ambao wameitwa kuhudumu kwa ubora mkubwa ndani ya kanisa, lakini hawatafuti kujulikana.
Lakini wapo wengine, wakifanya jambo lolote kanisani, wanataka kila mtu ajue.
Kwa mfano, mtu akiombea ibada siku ya Jumamosi na Jumapili kukawa na upako mkubwa, anaweza kujisifu akisema, “Ni kwa sababu nililala nikiomba jana usiku.”
Hata hivyo, Ufalme wa Mungu unajengwa pale kila mtu anapojua wajibu wake na kuutimiza kwa uaminifu. Hapo ndipo unakuwepo usikivu wa kile ambacho Roho Mtakatifu anafanya si kwa majivuno wala kujitukuza.
LUKA 15:1-7
“Watoza ushuru wote na wenye dhambi walikuwa wakimkaribia kumsikiliza Yesu. Mafarisayo na waandishi wakawanung’unikia, wakisema, ‘Mtu huyu huwakaribisha wenye dhambi, tena hula nao.’
Basi Yesu akawaambia mfano huu:
‘Ni nani kwenu mwenye kondoo mia, akipoteza mmoja wao, asiyewaacha wale tisini na kenda nyikani, aende kumtafuta yule aliyepotea hata amwone?’”
KULETA MAVUNO KATIKA UFALME
Moja ya matarajio makubwa ambayo Mungu anayo kwa sisi tuliookoka ni kuwaleta watu katika Ufalme Wake.
Sisi tuliookoka tunapaswa kutambua kuwa kuna watu huko nje wanaomhitaji Yesu, na ni jukumu letu kuwahubiria na kuwaongoza kwake.
Kila muumini anatakiwa awe na mtu mmoja angalau anayemlea ndani ya kanisa kila mwaka.
Huwezi kukaa kanisani mwaka mzima bila kumleta mtu yeyote kwa Yesu.
Ni lazima uwafikie watu na kushiriki nao Habari Njema za Yesu, kwa maana hii ndiyo kazi kuu tuliyopewa kama waamini.
Popote ulipo kazini, shuleni, katika familia au miongoni mwa majirani zako una wajibu wa kuwaleta watu kwa Yesu.
Kama vile mabalozi wa mataifa wanavyofanya kazi ya kuwavuta watu katika ufalme wao, vivyo hivyo, sisi kama mabalozi wa Kristo, tunapaswa kufanya kazi ya kuwaleta watu katika Ufalme wa Mungu.
KUZAA NA KUTUNZA MATUNDA
Fanya kila uwezalo kuzalia Mungu matunda na kuyatunza hayo matunda.
Ni jukumu lako kama mtoto wa Mungu kuleta mavuno.
Kanisa si mahali pa kufurahia tu na kushirikiana ni mahali pa kuandaliwa ili tuwafikie watu wanaomhitaji Yesu.
KAMA GARI LINALOHITAJI HUDUMA
Kila unapoinunua gari, unapewa idadi fulani ya kilomita za kuendesha kabla halijapelekwa service ili liendelee kufanya kazi vizuri barabarani.
Vivyo hivyo, sisi tuliookoka ni kama magari yanayopaswa kuwa barabarani tukiokoa nafsi, tukiponya wagonjwa, tukiwashauri watu, tukibadilisha maisha, na tukiwaleta watu kwa Yesu.
Tunaifanya kazi hii kuanzia Jumatatu hadi Jumamosi, na Jumapili tunarudi kanisani kwa service ili kutunzwa na kuandaliwa tena kwa kazi ijayo.
Hakuna gari linalopelekwa service halafu lirudishwe nyumbani lipakiwe tu likisubiri service nyingine.
Lakini ndivyo waamini wengi walivyo wanaenda kanisani kila Jumapili lakini hawafanyi kazi ya Mungu, hawawaleti watu kwa Yesu.
Sasa jiulize, wewe ni aina gani ya gari?
Ni lile linalofanyiwa service kila Jumapili lakini halitumiki kutimiza kusudi lake?
Kama kuanzia Jumatatu hadi Jumamosi hakuna mtu aliyeokolewa kupitia wewe, aliyeombewa na wewe, au aliyemjua Yesu kwa ushuhuda wako basi jukumu lako ndani ya kanisa ni lipi?
FAMILIA YAKO NDIYO SHAMBA LA KWANZA LA HUDUMA
Mashambulizi yoyote yanayotokea katika familia yako mara nyingi ni kwa sababu kuna mtu mmoja ndani ya familia ameruhusu mlango wa adui kufunguliwa.
Ikiwa unataka usalama, hakikisha familia yako yote imeokolewa ili adui anapokuja, asikute mlango wa kufunguliwa.
Ni jukumu lako kuhakikisha kila mtu anayeitwa kwa jina la ukoo wako ameokolewa.
Jiulize: Ni wangapi katika familia yangu ambao wamempokea Yesu?
Baadhi ya mapambano unayopitia ni kwa sababu wale wanaoshiriki damu na wewe ndio wanaokupinga kiroho wanatembelea waganga au wanafanya mambo ya giza.
Ni lazima usimame kwa ajili yao.
Omba na funga kwa ajili ya familia yako.
Mwambie Bwana kuhusu wao ili waokolewe, kwa maana wakisha okolewa, kila mlango wa ibilisi katika ukoo wako utafungwa.
JUKUMU LA MCHUNGAJI NA LA KONDOO
Siyo jukumu la mchungaji kulifanya kanisa likue.
Kazi ya mchungaji ni kulisha na kutunza kondoo, lakini kondoo ndio wanaozaliana.
Kanisa linapaswa kukua kwa sababu yako wewe.
Changamoto nyingi kazini zinatokana na ukweli kwamba watu unaofanya nao kazi hawajaokoka.
Uchawi na maovu mengine huendelea kazini kwa sababu hujawaleta watu hao kwa Yesu.
Ukiwashuhudia na wakaokolewa, hutaendelea kuhangaika kumtafuta mchawi, kwa maana watakuwa wamebadilishwa na nguvu ya Kristo.
JUKUMU LAKO
Unapowaleta watu wengi zaidi kwa Yesu wale wanaokuzunguka unafunga milango mingi ya adui ambayo ingeweza kutumika kukushambulia.
UKUMBUSHO WA MWISHO KWA WANAWAKE
Dada zangu, ni marufuku kuja mwakani bila waume zenu.