Mhubiri: Mtume Na Nabii Josephat Elias Mwingira
1. UTANGULIZI
Waefeso 2:13-18
“Lakini sasa, katika Kristo Yesu, ninyi mliokuwa mbali hapo kwanza mmekuwa karibu kwa damu yake Kristo. Kwa maana yeye ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi sote tuliokuwa wawili kuwa mmoja; akakibomoa kiambaza cha kati kilichotutenga. Naye akiisha kuuondoa ule uadui kwa mwili wake; ndiyo sheria ya amri zilizo katika maagizo; ili afanye hao wawili kuwa mtu mpya mmoja ndani ya nafsi yake; akafanya amani…”
Leo utaenda kuona amani ya moyo wako. Yote yaliyokukatisha tamaa lazima yawe na kikomo.
Mungu ni Baba yetu, naye ametupa nafasi ya kumkaribia.
Yeye ni kimbilio letu, nguvu yetu, na msaada unaopatikana wakati wa mateso.
2. DAMU YA YESU INATUPATANISHA NA BABA
Wakolosai 2:14-15
“Akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani; akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo.”
Tunaposogea katika msalaba, lengo ni kumkaribia Baba wa Mbinguni na kuondoa uadui uliokuwa umetutenga naye.
Kile kilichokutesa asili yake ikiwa ni dhambi kisogeze mbele za Baba yako wa mbinguni, nawe utakuwa huru.
Liko tumaini katika Mungu, kwa maana Yeye ndiye kimbilio letu.
Ametupa jina lipitalo majina yote jina la YESU.
Jina hili linaponya, linaokoa, linafungua, na lina nguvu kuu.
Tulitegemee jina hilo ili tuwe huru.
3. NGUVU YA JINA LA YESU
Matendo ya Mitume 4:7
“Walipowaweka katikati wakawauliza, Kwa nguvu gani na kwa jina la nani ninyi mmefanya haya?”
Ni kwa jina la Yesu na kwa nguvu za Mungu tunafanya mambo makuu.
Warumi 8:11
“Lakini, ikiwa Roho yake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu.”
Kila aliyeokoka ambaye Roho wa Kristo anakaa ndani yake, leo atahuishwa.
- Ikiwa kuna ugonjwa ndani yako unaokuangamiza, leo utaondoka.
- Kiungo chochote kilichokufa katika mwili wako, kifufuliwe kwa jina la Yesu.
- Kama ni kisukari, kansa, au mifupa iliyovunjika Bwana ataiunganisha na kuhuisha misuli yako.
Jiandae kuinuka tena, kwa maana Roho Yule aliyemfufua Yesu anakaa ndani yako.
4. UHURU KATIKA JINA LA YESU
Kila nira iliyokufunga ivunjike sasa kwa jina la Yesu.
- Ugonjwa usalim amri.
- Mapepo, majini, vibwengo na laana vikutoke sasa kwa jina la Yesu.
- Kila uchawi, kila maneno ya laana yaliyotamkwa juu yako yakose nguvu.
Uwezekano ni huu: unaweza kuwa na ugonjwa ambao hata madaktari hawaelewi;
lakini leo ugonjwa huo utatiishwa chini ya jina la Yesu, kwa maana hakuna jina lililo juu ya jina lake.
Ukawe huru kwa jina la Yesu.
5. YESU MFALME WA AMANI NA NGUVU
Isaya 9:6
“Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, tumepewa mtoto mwanamume; na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; naye ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani.”
Kama anayekutesa ni mfalme wa giza, basi yupo Mfalme wa Nuru atakayekuangaza.
- Kama kuna jambo halieleweki katika maisha yako, Bwana atakushauri.
- Huo ugonjwa unaokutesa, maisha yanayokulemea, mizimu ya ukoo, matatizo ya watoto au wazazi wako mpe Bwana.
Yeye anaweza yote.
Kama kuna miungu ya mababu inayosababisha mateso, mkaribie Mungu mwenye nguvu naye atakupokea na kukuokoa.
6. MUNGU ANAPONYA NA KUSAMEHE
Zaburi 103:1-3
“Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana. Naam, vyote vilivyo ndani yangu vilihimidi jina lake takatifu. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana, wala usizisahau fadhili zake zote. Akusamehe maovu yako yote, akuponya magonjwa yako yote.”
Kama umesamehewa, basi uponyaji ni haki yako.
Hata kama ugonjwa ni wa mauti, hata kama wamepanga ufe kesho hutakufa, kwa jina la Yesu.
Mungu amekupa siku za kuishi; na iwe hivyo kwako kwa jina la Yesu.
7. NINI KINAENDA KUFANYIKA
- Omba kwa ajili ya afya yako isikutane na ugonjwa wowote hadi siku ya kuondoka duniani.
- Omba kwa jina la Yesu kuvunja kila nira, laana, na nguvu za giza.
- Shukuru Mungu kwa amani, uponyaji na uhuru aliokupa leo.
8. HITIMISHO
Yesu ndiye Chanzo cha Amani na Uponyaji Wetu.
Anapofika katika maisha yako, uadui huondoka, dhambi hufutwa, na mwili huponywa.
Tumaini lako lisiwe kwa mwanadamu, bali kwa Yesu Kristo pekee, jina lipitalo majina yote.