KUISHI MAISHA YA UTII, UAMINIFU NA KUJITOA.
UTII maana yake ni kukubali na kutendea kazi maagizo. Utii una maumivu kwa sababu haukupi kufanya kile unacho taka wewe bali unatakiwa kufanya kile ulicho amriwa kufanya.
Kumbukumbu la Torati 28:1, "Itakuwa utakaposikia sauti ya BWANA, Mungu wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo BWANA, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya duniani."
Isaya 1:19-20, "Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi; bali kama mkikataa na kuasi mtaangamizwa kwa upanga; maana kinywa cha BWANA kimenena haya."
Tunajifunza kuwa asili ya baraka zote ni utii. Anaye bariki ni MUNGU mwenyewe baada ya kuwa na uhakika wa tabia yako ya kutii. Siyo baraka tu, hata mamlaka ya MUNGU inafanya kazi katika kanuni hiyo hiyo ya utii.
Yakobo 4:7, "Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia." Kwa hiyo ni lazima ujikague na kujiuliza juu ya kiwango chako cha UTII kuhusu matakatifu ya MUNGU kila wakati.
UAMINIFU ni hali ya mwenendo na tabia binafsi ya kufanya kwa utii na unyenyekevu kwa kutunza na kutenda kila neno lililo agizwa. Mwaminifu hawezi kuiba fungu la kumi maana anajua kwa kufanya hivyo atachuma laana. Mwaminifu hutunza na kutimiza ahadi na wajibu wake.
KUJITOA ni kuwa tayari kutumiwa kwa ajili ya BWANA. Warumi 12:1, "Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana."
Ifike mahali uwe tayari kujigharimu kwa ajili ya MUNGU. Tabia hiyo inampa MUNGU utukufu na ndiyo maana imefananishwa na dhabihu iliyo hai tena takatifu.
-:MTUMISHI ANNA JOSEPHAT MWINGIRA- KANISA LA EFATHA.
... See MoreSee Less