NENO LA SIKU.
Na Mtume na Nabii Josephat Elias Mwingira, Kanisa la Efatha.
Tarehe 16/10/2024.
Mathayo 24:13 “Lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka.”
Wabeba ndoto wana vizuizi vingi sana kutoka kwa wapinzani wao. Kabla ya kuona ndoto yako ikitimia kuna maumivu mengi utapitia ili hiyo ndoto ipate kutimia, kwa sababu NDOTO ni kama mtoto akitoka katika tumbo la mama yake. Usiwe na mashaka unapopitia maumivu ili kuifikia ndoto yako kwa sababu upo katika Njia sahihi.
Kabla ya Yusufu kuifikia ndoto yake, alipita kunako maumivu mengi; alitaka kuuawa na ndugu zake, aliuzwa utumwani, alifungwa gerezani lakini aliishia kuwa mtu mkuu sana na akawa msaada kwa ndugu zake. Yesu kabla ya kuifikia ndoto yake, alipitia msalaba na akapigwa misumari; lakini sasa YEYE ni BWANA wa MABWANA na anatawala dunia nzima.
Mwana wa Mungu unapokuwa katika safari ya kuiendea ndoto yako vizuizi na vipingamizi ni vingi sana ili tu usifikie katika ndoto yako, lakini usikate tamaa, pigania ndoto yako mpaka itimie.