Kujitambua

Kujitambua
MTUME NA NABII JOSEPHAT ELIAS MWINGIRA
Tunaenda ibadani na kufanya kila kinachohusu kanisa, hayo yote ni maandalizi ya kwenda kule tunakotamani kwenda.
Yesu aliweka mfano na kusema; Ufalme wa Mungu unafananishwa na wanawali kumi, watano wenye busara na watano wapumbavu. Kanisa ni bibi harusi wa mwana kondoo, lengo la kuwa bibi harusi ni ili kuandaa watu waweze kujua kuwa kuna siku watatakiwa na Bwana wao. Katika mambo yote lazima ujue wewe uliyeokoka ni bibi harusi lakini katika ma bibi harusi wale kumi waliokuwa wanamsubiria Bwana Yesu, watano walikuwa ni wapumbavu na watano ni wenye busara. Je! Wewe uko wapi hapo?
Utajuaje kama wewe ni mpumbavu au una hekima? Wale wanawali 10 walikuwa wakimsubiri Bwana harusi wakiwa wameshika taa ziko tayari kumsubiria Bwana harusi ili wapate kuingia ukumbini kwa harusi lakini watano wanamafuta na watano hawana mafuta, kuna watu leo hii wako kanisani na wameokoka na wananena kwa lugha lakini hawana mafuta. Kumbe taa unayo kwa maana umeokoka, lakini hoja ya Yesu haikuwa kwenye taa wala bibi harusi, bali ilikuwa ni kwenye kujitambua; je! Wewe mafuta yako yapo wapi?
Bartimayo alipokuwa akipaza sauti yake kumuita Yesu, wanafunzi wa Yesu walimnyamazisha, lakini hakuwasikiliza wao kwa maana lengo lake lilikuwa ni kukutana na Yesu na siyo wanafunzi wa Yesu. Unapokuwa katika kumuita Bwana wa mabwana usiridhike na mtu yeyote anayekwambia nyamaza, usikubaliane na mtu yeyote anayekwambia hauwezi, haufai, haukubaliki; kwa sababu ulipookoka haukumjia huyo anayesema hayo bali umemjia mmoja tu anayeitwa Bwana wa mabwana; Baba wa milele Mungu mwenye nguvu na mfalme wa Amani, huyo ndiye uliyemjia muangalie yeye tu na siyo wanadamu.
Waebrania 10:7 “Ndipo niliposema, Tazama, nimekuja (katika gombo la chuo nimeandikiwa) Niyafanye mapenzi yako, Mungu.”
Kabla haujamiliki kitu chochote kwanza mfanye Mungu awe wa kwako kwa maana usipofanya hivyo usitarajie kumiliki chochote, ni mpaka utakapokuwa umemmiliki Mungu ndipo utaona ustawi kwako.
KUJITAMBUA:
Hii ndiyo siri namba moja ya kukufanya wewe upate kumiliki; .je! Wewe ni nani? Lazima ujitambue kwa maana usipojitambua kamwe hautaweza kumtambua yule aliyekuumba. Kwa kadri unavyojitambua mwilini ni lazima ujitambue na rohoni wewe ni nani. Kwa maana utambulisho wako ndiyo utakaokupa kumiliki au kutokumiliki. Jitambue kwanza ili upate kumiliki.
Waebrania 10:7 “Ndipo niliposema, Tazama, nimekuja (katika gombo la chuo nimeandikiwa) Niyafanye mapenzi yako, Mungu.”
Mstari huu unaonesha kujitambua, wacha kulia lia pindi pale mambo yanapotokea kwako; chukua nafasi yako kwa maana ukianza kulia ni dalili ya kushindwa.
Mtu aliye na Yesu halii kwa sababu amesemwa vibaya, au amenyang’anywa kitu, hapana! Wao wakitengeneza tukio lao wewe tengeneza tukio lako ambalo litafunika yale waliyofanya na usonge mbele. Daudi kila alipofika akikuta tukio alikuwa anatengeneza tukio lake na linakuwa ni la Ushindi; kwa nini wewe unalia lia? Tengeneza tukio.
Habakuki 2:1 “Mimi nitasimama katika zamu yangu, nitajiweka juu ya mnara, nitaangalia ili nione atakaloniambia, na jinsi nitakavyojibu katika habari ya kulalamika kwangu.” Hapa hakusema Askofu, Mchungaji wala mama wa maombi ndiyo anaweza kupeleka maombi mbele za Mungu wako, la! Bali wewe unapaswa kusimama katika zamu yako na Mungu atakusikia.
Mwana wa Mungu unapaswa kutambua kuwa maombi yako yanasikika zaidi kuliko ya mtu yeyote yule akiomba kwa ajili yako, kwa sababu ukimuelezea mtu anaweza kueleza sawa sawa na ulivyomueleza, lakini wewe ukienda mwenyewe mbele za baba wa mbinguni atakusikia Zaidi. Mchungaji au Askofu akiomba kwa ajili yako na hilo jambo likatokea ni kwa Neema, ambayo hata wewe mwenyewe unayo, jitambue na usimame kwenye zamu yako. Wewe ndiye mwenye maamuzi ya kile kinachoendelea katika maisha yako, fanya maamuzi.
Kazi unayoifanya, ndoa uliyo nayo au biashara yako kama inakupa furaha ya kumwabudu Mungu basi ni ya Mungu lakini kama inakunyima kumfanyia ibada Mungu wako basi sio ya Mungu. Simamia kile unachokijua ili uweze kumpendeza Mungu.
Iwe ni kazini, kweye biashara yako au popote pale ulipo acha wajue kuwa wewe ni wa Mungu wakimchukia Mungu wako jua kuwa wao hawana Mungu.
Binti na kijana jitambue, ili umpate mtu sahihi katika maisha yako,
Kwasababu umeshindwa kujitambua ndiyo maana haustawi kwa maana Mungu hawezi kumpa mpumbavu. Usitafute kubembelezwa.

Add Comment