Somo: Mbaraka

Somo: Mbaraka
Mtume na Nabii Josephat Elias Mwingira
A. Umiliki wa mwanadamu; Hatuwezi kuzungumzia Baraka pasipo kuelewa nafasi ya mwanadamu; Nafasi ya mtu itamuhakikishia mtu huyo nini anachoweza kumiliki. Mwanzo 1:26-27 “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.” Nafasi ya mtu ni lazima iungamane na muumbaji, pasipo hilo kumiliki ni kitu kigumu kwa huyo mtu.
B. Baraka ni nini? Ni neno lililotamkwa kwa uumbaji; Mungu alitamka neno kwa kiumbe kilichoumbwa na kwa kupitia hilo neno hicho kilichoumbwa mbaraka uliamriwa kwake. Kwa maana hiyo tunaona mbaraka siyo vitu bali ni neno la amri lililotamkwa ambalo mara zote hukutangulia na kuandaa mazingira kwa ajili yako.
AINA ZA BARAKA
• Mwanzo 1:28 “Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi.” Hapa tunamuona Mungu aliamuru Baraka kwa mwanadamu kwa kupitia Neno lake na ikawa.
• Mwanzo 2: 1-3 “ Basi mbingu na nchi zikamalizika, na jeshi lake lote. Na siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyoifanya; akastarehe siku ya saba, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoifanya. Mungu akaibarikia siku ya saba, akaitakasa kwa sababu katika siku hiyo Mungu alistarehe, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoiumba na kuifanya.”
Hapa tunaiona, yakupasa kuibariki siku ili izalishe Baraka, tunapo amuru Baraka za siku maana yake tunaamuru hiyo siku kuzalisha vinavyo ambatana na hiyo siku.
Kila siku inakitu cha kipekee kwa ajili yako, kwa maana hiyo kama siku haijabarikiwa basi hauwezi kupata hiyo Baraka. Kila siku ni siku ya Mungu, siku unapopata siku yako ndipo unapokuwa umebarikiwa. Kila baraka ina siku yake ukijua kuhesabu siku zako ndivyo unakuwa tajiri, lakini ukiikosa siku ndivyo unavyokuwa masikini ilihali umebarikiwa, unakuwa umebeba Baraka lakini hauna hizo Baraka.
Kwa Mungu kuna kila aina ya Baraka, ukitaka watoto, elimu, mume au mke, pesa zipo kwa ajili yako lakini ukikosa kuijua siku yako ambayo hiyo Baraka yako imeachiliwa basi hautaweza kuipata hivyo unapaswa kuwa makini sana. Siku yako lazima ibarikiwe.
Huu ni mwisho wa mwaka, ni wiki na Jumapili ya mwisho wa mwaka 2024, Hii ni Jumapili itakayokuhakikishia ni kwa jinsi gani utaingia mwaka 2025 Mwaka huu ni mwaka wa kumiliki, je wewe uliumilikije? Tutakwenda kuona mwaka 2025 kwa sababu tutaona namna unavyoabudu, unavyohusiana, familia yako unaendeshaje na maisha yako pia.
Uhakikisho wa leo ni huu kamwe hutakufa mpaka uione 2025. Inawezekana upo kitandani leo hii au upo hospitalini unaumwa, hakuna hukumu ya kifo itakayokupelekea katika umauti, yeyote atakayeisikia sauti yangu leo atafika kule ambapo Mungu anataka afike.
Mwanzo 12:1-3 “Bwana akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha; nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka; nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa.”
Hii ni aina nyingine ya Baraka ambayo unaanza kutengwa na baadhi ya watu kutokana na tabia zao, aina hii ya Baraka unaipata kupitia tabia yako.
Ukiwa na tabia ya kumpendeza Mungu anakuchagua na kukutenga, hapa ndipo wateule walipoanza, huu unaitwa mbaraka wa wateule, na ndiyo maana katika Biblia tunarithi mbaraka wa Abrahamu kwa sababu Abrahamu alichaguliwa na kutengwa na sisi tumechaguliwa.
Mbaraka ulikuja hapa baada ya mambo mawili;
1. “Bwana akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha;” Mungu alimuamuru Abrahamu atoke katika nchi yake ili wengine wasije kuharibu mbaraka wake. Tabia yako itasababisha mbaraka ukufuate popote uendapo au la.
2. “Nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako;” Kwa wateule ili waweze kumiki mbaraka huu ni lazima wamiliki hiyo amri, ambayo iwakutoa katika mahali walipo pazoelea waende katika Baraka zao, Baraka zako zitakufuata huko uliko, wewe umebarikiwa sana.
MBARAKA WA UBABA KUTOKA KWA MTUME NA NABII JOSEPHAT ELIAS MWINGIRA
Kuanzia leo nenda Ukazae na Kuongezeka, katawale uumbaji, na Amuru Baraka za Mungu zile ambazo anawapa wale awapendao zikakujilie wewe. Naamuru mbaraka wa Mungu ukawe juu yako na ule unono wa Nchi uje na kudumu katika maisha yako, Mungu akakupe kuishi na kuongezeka.
Naamuru siku ya leo Mungu akakupe kukaa salama na kufurahi katika siku zako zote ulizopewa na Bwana, kisiwepo kitakachoinuka kinyume chako na kuondoa usalama wako au furaha yako. Mungu akakutegemeze kwa wepesi katika yote unayoyafanya. Kuanzia leo magonjwa na maradhi siyo sehemu yako tena, Bwana akakupe afya njema siku zote za maisha yako, kuanzia leo Mungu akaridhie mawazo ya moyo wako na kuyabariki.
Kuanzia leo kazi ya mikono yako ikupe faida. Kuanzia sasa kizazi cha uovu kikakae mbali na wewe, jina la Yesu Kristo likawe rungu lako la kuponda adui zako. Kuanzia sasa naamuru yaliyo mbali yakakusogelee, yaliyokimbia au yaliyoshindikana yakakufute ulipo. Natangaza vyote ulivyo poteza vinaenda kukurejea kwa maana Bwana anakwenda kukurejeshea, vile vitamanikavyo vikawe sehemu ya maisha yako. Uovu hautakukaribia, Bwana anakwenda kukugeuza moyo wako na akili yako ipate kumwandama Yeye.
Maisha yako hayatakuwa yako tena bali yataongozwa na Bwana siku zote za maisha yako. Kuanzia sasa hutakufa mapema utakuwa faraja kwa familia yako, Taifa lako na kwa Kanisa maana Bwana amekuridhia.
Natangaza siku hii ya leo, Bwana akaridhie Malaika wake waanze kuongoza hatua zako mpaka pale ambapo Yeye ameandaa mema yako, mazuri yako, Matakatifu yako na makuu yako. Malaika wataongoza miguu yako hautaenda kushoto wala kulia bali watakufikisha kule ambako Mungu amekuandalia.
Kuanzia leo umeinuiliwa, mwisho wako utakuwa bora kuliko mwanzo, waliokucheka, waliokudharau watajua wewe umekumbukwa na Bwana. Leo ni mwisho wa msiba wako, kudharauliwa, kushindwa, utaanza biashara na laki moja utaishia kuwa bilionea, maana kushindwa kumeondolewa kwako.
Kuanzia leo nenda Ukazae na Kuongezeka, katawale uumbaji, naamuru Baraka za Mungu zile ambazo anawapa wale awapendao zikakujilie wewe. Naamuru mbaraka wa Mungu ukawe juu yako na ule unono wa Nchi uje na kudumu katika maisha yako, Mungu akakupe kuishi na kuongezeka.
Kuanzia leo umeinuiliwa, mwisho wako utakuwa bora kuliko mwanzo; waliokucheka, waliokudharau watajua wewe umekumbukwa na Bwana. Leo ni mwisho wa msiba wako, kudharauliwa na kushindwa.
Kuanzia sasa hutakufa mapema utakuwa faraja kwa familia yako, Taifa lako na kwa Kanisa maana Bwana amekuridhia.

Add Comment