Somo: Mwaka wa kumiliki

Somo: Mwaka wa kumiliki
MTUME NA NABII JOSEPHAT ELIAS MWINGIRA – KANISA LA EFATHA
SOMO: MWAKA WA KUMILIKI
Mathayo 6:33 “Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.” Hii ina maana kuwa chochote ufanyacho kwanza tafuta ufalme wa Mungu.
Chochote unachotaka kutafuta au kugundua katika maisha yako tafuta kwanza ufalme wa Mungu, kama unataka kuanzisha jambo au unataka kufunga ndoa tafuta kwanza ufalme wa Mungu; kama unataka uwe na watoto, ujenge nyumba au kuishi Maisha mazuri tafuta kwanza ufalme wa Mungu ili hivyo utakavyovipata viweze kudumu katika maisha yako.
Kwa maana chochote unachokitaka chanzo chake kipo katika kutafuta kwanza ufalme wa Mungu, ukishindwa kutafuta kwanza huo ufalme maana yake chochote utakachokipata utapokonywa.
Ukitaka uwe na amani na furaha na uwe na uzima wa milele na maisha mema na yenye ustawi, basi tafuta kwanza ufalme wa Mungu. Chakwanza kinakuwa chakwanza kama hauna cha kwanza basi utaanza na cha pili au cha tatu, namba yoyote utakayoipokea pasipokuwa na namba ya kwanza kamwe haitaweza kudumu kwako.
Pasipo Mungu kwanza au ufalme wa Mungu basi elewa kuna ufalme wa giza.
Huku duniani kuna ufalme wa nuru na wa giza; nuru ndiyo tunaiita kwanza, giza ndiyo namba mbili hivyo maamuzi ni yako unataka kutembea na nuru au giza, je! Wewe unataka kutembea na nini? Lakini mashauri ninayokupa, chochote unachotaka kupata au kufanya lazima uanze na kwanza yaani nuru ili uweze kuongeza la pili na tatu ambazo ni Baraka kwako.
Mathayo 6:33 “Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.”
Ukiwa hauna cha kwanza chochote utakachokipokea kitachukuliwa, na ndiyo maana Bwana Yesu akasema “yeyote aliyenacho ataongezewa na yeye ambaye hana hata kile kidogo alichonacho kitachukuliwa” kwa nini? Kwa sababu alianza bila kuwa na cha kwanza.
Kama ndoa yako ilianza bila Mungu itang’olewa hata ukiishikilia vipi maana haina Mungu.
Chochote unachokitaka Mungu anakitaka pia hivyo tafuta kwanza ufalme wa Mungu ili YEYE apate kukuzidishia yale unayoyataka katika maisha yako.
Katika kumiliki mali zetu kuna mambo ya kuzingatia, hakikisha unazingatia haya:
1. Hakikisha umeoshwa kwa damu ya Yesu (umeokoka), Waefeso 2:13 “Lakini sasa, katika Kristo Yesu, ninyi mliokuwa mbali hapo kwanza mmekuwa karibu kwa damu yake Kristo.”
2. Upatanishwe na Mungu; hakikisha hakuna uadui kati yako na Mungu, Mungu ana Amani na wewe uwe na Amani na Mungu. Waefeso 2:16 “Akawapatanisha wote wawili na Mungu katika mwili mmoja, kwa njia ya msalaba, akiisha kuufisha ule uadui kwa huo msalaba.”
Amani ya Mungu itakufanya uwe na furaha, unafurahia kusoma neno na kuomba na utafurahia mambo ya Mungu, unafurahia kwenda kanisani na kutoa sadaka kwa sababu una Amani na Mungu wako, huhitaji mtu akusukume ili uweze kufanya jambo kwa Mungu.
3. Lazima uwe raia wa Mbinguni; Waefeso 2:19 “Basi tangu sasa ninyi si wageni wala wapitaji, bali ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake Mungu.”
Utajuaje kuwa sasa wewe ni raia wa Mbinguni?
Muda wote unapata ndoto; unaona maono, unapenda kuomba, kusoma Neno la Mungu na unapenda kuona watu wakikombolewa na wakiokolewa.
Utakuwa jasiri na hodari wa kusema na kushuhudia habari za Mungu pasipo hofu wala woga.
4. Upandwe na ujengwe katika nyumba ya Bwana, Waefeso 2:20 “Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni.” Unapojawa na furaha ya kusikiliza mafundisho ya kitume, kuongozwa na Mitume na Manabii; mbingu itaweka alama kuwa wewe ni wa muhimu sana katika ufalme wa Mbinguni.
Zaburi 1:3 “Naye atakuwa kama mti uliopandwa Kandokando ya vijito vya maji, Uzaao matunda yake kwa majira yake, Wala jani lake halinyauki; Na kila alitendalo litafanikiwa.” Utawezaje kuwa uliyepandwa? Muda wote utatamani kumsikiliza Roho Mtakatifu, popote utakapokuwa unapenda kunena kwa lugha, unawasiliana na mbingu wakati wote.
5. Uwe katika roho na ujionyeshe pale Mungu alipo, hakikisha unaishi katika roho. Waefeso 2:18 “Kwa maana kwa yeye sisi sote tumepata njia ya kumkaribia Baba katika Roho mmoja.” Haendi karibu na Baba wa mbinguni kwa kulia, la! Bali kwa kuwa katika roho. Kwa nini uwe katika roho? Kwa sababu unajiwakilisha katika uwepo wa Mungu.
6. Hakikisha unaweza kuingia na kutoka ili uweze kupokea kile unachokihitaji kutoka kwake. Yohana 10:9 “Mimi ndimi mlango; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata malisho.” Unaingiaje na kutoka? Unaponena kwa lugha unaingia, unapomaliza kuchukua kile unachotaka kuchukua katika roho ndipo unatoka na nguvu ambayo itakupa uwezo wa kumfukuza ibilisi katika maisha yako.
Mtoe ibilisi katika maisha yako katika kile unachotaka kumiliki, kwa maana hauwezi kumiliki kama ibilisi akiwa katika mazingira yako mtoe kwanza. Kama unataka kumiliki biashara kubwa jua kuwa hiyo biashara ina ushindani mkubwa hivyo unaihitaji nguvu ili uweze kushinda.
7. Hakikisha unafanya ulichoagizwa, Yohana 15:14-15 “Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo. Siwaiti tena watumwa; kwa maana mtumwa hajui atendalo bwana wake; lakini ninyi nimewaita rafiki; kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu.” Ukiwa rafiki wa Yesu hakuna siri tena ambayo hautaijua, wewe omba yeye atakwambia.
8. Tupendane sisi kwa sisi; Yohana 13:34-35 “Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo. Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi.”
9. Hakikisha unawafanya watu kuwa wanafunzi wa Yesu; Mathayo 28:19-20 “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.” Hii ndiyo amri tuliyopewa sisi wana wa Mungu, ukisha litimiza ndipo sasa unaweza kuomba lolote na ukapewa. Tafuta kwanza, ukitafuta kwanza maana yake umetii amri yake hivyo unapozingatia ndipo sasa Mungu anaruhusu uwe rafiki wa mwanaye (Yesu Kristo) na kuanzia hapo omba lolote nawe utapewa.
10. Omba lolote nawe utapewa.

Add Comment