Umiliki wa wana wa Mungu

Umiliki wa wana wa Mungu
KATIBU MKUU WA KANISA LA EFATHA PROFESSOR EMMANUEL CHAO
Biblia inatukumbusha ya kwamba milki na urithi wote wa wana wa Mungu umefungwa ndani ya ufalme wa Mungu na hakuna chochote kinachoweza kupatikana nje ya huo ufalme. Unapozidi kuuelewa ufalme wa Mungu ndipo unakuja na mema yake yaliyofungwa nayo.
Wakolosai 1:12 “Mkimshukuru Baba, aliyewastahilisha kupokea sehemu ya urithi wa watakatifu katika nuru.” Urithi wetu umehifadhiwa ndani ya nuru na hauwezi kuchangamana na kitu chochote kilicho nje ya nuru.
Waefeso 1:13-14” Nanyi pia katika huyo mmekwisha kulisikia neno la kweli, habari njema za wokovu wenu; tena mmekwisha kumwamini yeye, na kutiwa muhuri na Roho yule wa ahadi aliye Mtakatifu. Ndiye aliye arabuni ya urithi wetu, ili kuleta ukombozi wa milki yake, kuwa sifa ya utukufu wake.” Chochote kinachohusu umiliki wa wana wa Mungu ni utimilifu aliyouandaa Mungu kwa ajili ya kuleta ukombozi wa milki kwa watu wake.
Unapo miliki siyo kwa ajili yako bali ni kwa ajili ya ufalme wa Mungu; balozi yeyote akitoka nje ya nchi yake na akanunua ardhi kwa ajili ya nchi aliyotoka lile eneo haliwi la kwake pamoja na kuwa anamiliki hapo lakini hilo eneo linakuwa ni mali ya nchi aliyomtuma. Sisi tuliyookoka ni mabalozi wa Kristo, tunauwakilisha ufalme wa Mungu hapa duniani. Mungu anapo zungumzia sisi kumiliki siyo mjadala wako wewe bali wewe unapaswa kufungua ufahamu wako na uelewe lugha inayozungumzwa hapo kuwa ni lugha ya kifalme na ya kuwa huo umiliki ni halali yako ili uweze kuupata.
2 Mambo ya Nyakati 1:7 -12 “………Naye Mungu akamwambia Sulemani, Kwa sababu neno hili lilikuwamo moyoni mwako, wala hukujitakia mali, wala utajiri, wala utukufu, wala maisha za wakuchukiao, wala hukujitakia maisha ya siku nyingi; bali umejitakia hekima na maarifa, upate kuwahukumu watu wangu, niliokutawaza juu yao; basi hekima na maarifa umepewa; nami nitakupa mali, na utajiri, na utukufu, kupita walivyokuwa navyo wafalme wote waliokuwa kabla yako, wala baada yako hapatakuwa na mtu atakayekuwa navyo.”
Wakati Mungu anamuuliza Suleiman swali hakujiandaa kujibu bali alijibu yale yaliyo moyoni mwake, hilo ndilo lilikuwa ni tamanio la Suleimani na hilo tamanio likampa yeye kumiliki yote.
Sababu ya suleimani kutaka hekima kwa Mungu ilikuwa ni nini? Ilikuwa ni kipaumbele chake, Suleiman kipaumbele chake kilikuwa sio kupata hekima na maarifa ili awe mfalme mashuhuri sana katika ufalme wake, La! bali ilikuwa ni ili aweze kukitunza kile Mungu alichompa ambacho ni ufalme pamoja na watu wake.
Huu ni mwaka wetu wa kumiliki na tumetangaziwa kumilki lakini tukikuuliza kwa nini unaitaka hiyo milki utasema ni kwa sababu huu ni mwaka wa kumiliki; lakini unapaswa kutambua kuwa hautaupokea huo umiliki ikiwa tu nia yako ni tofauti na nia ya Mungu. jambo hili linaweza kuonekana ni jepesi sana lakini linabeba makusudio ya Mungu kwako.
Moyo wa mtu ambaye hajaandaliwa ukikutana na nguvu ya ufalme unaleta uharibifu mkubwa sana.
Yesu akasema katika Mathayo 6:33 “Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.” Unahitaji kuupokea kwanza ufalme ili uweze kupokea haki iliyopo ndani ya huo ufalme pia.

Add Comment