NENO LA SIKU.
Na Mtume na Nabii Josephat Elias Mwingira, Kanisa la Efatha.
Tarehe 14/10/2024.
Zaburi 23:5 “Waandaa meza mbele yangu, Machoni pa watesi wangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, na kikombe changu kinafurika.”
Mungu amekukusudia kumiliki ndani ya Mwaka huu wa Kumiliki, lakini meza yako imeandaliwa mbele ya adui zako, pale ambapo watesi wako wapo, sasa usipowashughulikia hao adui zako kamwe hautaweza kumiliki yale yaliyo ya kwako.
Mungu akawaambia wana wa Israel amewapa nchi ya maziwa na asali, wapi? Hapo ambapo kuna majitu, walipofika mahali wakakata tamaa na kujiona wao ni kama panzi mbele ya hayo majitu hawakuweza kuirithi ile nchi, ni watu wawili tu ambao walikuwa na moyo wa imani ndio waliyoingia katika ile nchi ya ahadi ambao ni Joshua na Kalebu, lakini wote waliotoka Misri jeshi lote lilifia jangwani.
Wewe umepewa Kumiliki na Mamlaka hiyo ipo juu yako itendee kazi sasa, lakini kama unasubiri Yesu akemee mchawi aliyeko kwenu basi utakaa sana, kama unamsubiri Yesu akemee mzimu wa babu yako utakufa masikini, lakini kama unajua kuwa Yesu amekupa Mamlaka na ukasimama na hiyo Mamlaka basi utakuwa Mshindi siku zote.
Luka 10:19 “Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru.” Simama katika nafasi yako ili uweze Kumiliki.