Wazo la Mungu kwako

Wazo la Mungu kwako
MTUME NA NABII JOSEPHAT ELIAS MWINGIRA
Wazo la Mungu kwetu lilikuwa ni hili; Mwanzo 1:26 “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.”
Hili ndilo wazo la Mungu kwa mwanadamu aliyemuumba. Ili tuweze kufikia makusudi ya kuishi kwetu hapa chini ya jua ni lazima tuelewe ilikuwaje mpaka sisi tukawa huku duniani.
Katika mstari huu wa Biblia tunamuona Mungu akisema kwa habari zako na sio habari za mtu mwingine, siku ukielewa na kuliweka hili katika akili yako hivi vituko vya duniani na maisha magumu unayopitia hayatakuwepo, unaolewa na unaachika au unaoa unaacha mke kwa sababu haujaelewa hapo. Unafeli shuleni ni kwa sababu haujaelewa hapo, unafeli katika biashara yako kwa sababu haujaelewa hapo, utakufa mapema kwa sababu haujaelewa hapo. Lakini siku ukielewa hakuna kitu kitaenda tofauti katika maisha yako.
Mwanzo 1:26 “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.”
Hii ina maana kuwa kila kilichopo hapa chini ya jua kimefanywa kwa sababu ya sisi wanadamu, chochote unachokiona huku duniani kilicho hai au kimekufa umepewa wewe mwanadamu, hata fedha pia umepewa wewe, sasa kwa nini inakusumbua? Siku ukielewa kuwa Mungu amekuumba ili uwe mtawala huku duniani basi umepokea kile alichokukusudia.
Biblia inasema kuwa “Mungu akasema” chochote Mungu alichokisema kilikuwa na wewe, je Mungu alishawahi kusema kitu na hakikutokea? Hapana, sasa kwa nini wewe ukisema kila kitu hakitokei?
Mungu alimuumba mtu kwa sura na mfano wake, hivyo mwanadamu ni sura na mfano wa Mungu; Mungu anasema na inakuwa; sasa je! Kwa nini wewe uliye sura na mfano wake unasema na haiwi? Je! Wewe unafanana na nani? Watu wanaofanana na Mungu wanafanya ya Mungu, je! Wewe unafanya ya Mungu?
Mwanzo 1:26 “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.”
Kuongea, kuzungumza na kusema ni vitu vitatu tofauti, Mungu hazungumzi wala haongei bali anasema.
Unapoongea au kuzungumza na mtu ni kama mahojiano, ni mashauri, ni kama unatoa nasaha, lakini kusema ni amri, yaani ni namna ya kusababisha kitu kitokee.
Mfano: Unaona duka lako haliendelei, sema jambo juu ya duka lako na siyo kuongea kuwa biashara ni ngumu, sema jambo kwa ajili ya mwanao, sema neno juu ya ndoa yako, kusema maana yake ni kuamrisha kitu kipate kutokea, lakini watu wengi wanaongea hawasemi na ndiyo maana mambo hayatokei kwao, kwa sababu kusema kunatokana na mtu anayejua ana mamlaka na uwezo gani juu ya hicho kitu anachopitia, sasa wewe unaona kabisa kuwa una mamlaka juu ya kitu lakini unazungumza au unaongea matatizo yako hapo usitarajie kupata matokeo katika hicho kitu unachoongea. Ikifika kwa habari ya mamlaka tuliyonayo tunasema ili kuruhusu jambo litokee.
Unakuta mtu amefungua duka halafu anaenda asubuhi na kusema “unajua tangu juzi sijauza” ukisema hivyo umesha lilaani hilo duka lako; maana umeamrisha lisizae.
Ikifika saa ya kusema lazima kwanza ujue unataka nini au unatamani nini ndipo unasema, siyo unasema maumivu yako, kwa maana ukisema maumivu yako kamwe hayatakaa yaishe.
Mathayo 6:9-13 “Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje, Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni…….”
Kwanza unapaswa kujua ni kwa jinsi gani unaweza kulitukuza jina la Bwana, inabidi ufanane naye kwanza, hata wanafunzi wa Yesu walipokuwa huku duniani walifanana na Yesu katika kuongea, kutembea na kila kitu, sasa wewe uliyeokoka, unapaswa kufanana na Bwana wa mabwana.
Kabla mambo yako haujayaanza unapaswa kutambua haya:
1. Jina lake kwanza; jina lake lina nini? Ni takatifu, ni kweli, hivyo yote yanayoambatana na hilo jina lazima yawe ndiyo tabia yako,
2. Lazima ujifunze kusababisha ufalme wa Mungu uje; lazima uangalie ni nini kinafanana na ufalme wa Mungu, soma Biblia na uelewe ni mambo gani ya ufalme na uyatekeleze hayo kwa maana ukifanya hayo utasababisha ufalme ufanane na wewe.
3. Mapenzi yake; lazima usimame na utimize mapenzi ya Mungu.
Mwanangu mazuri yako yapo mbele yako, hivyo wewe kazi yako ni kuyachukua, yachukue sasa kwa jina la Yesu.
Katika safari hii ya kuyaendea yale mema yako kunahitajika uhodari na ujasiri kwa sababu utakutana na pingamizi njiani; kuna vitu vitakuvuta nyuma, hivyo unahitaji ujasiri na uhodari ili lolote litakalokuja mbele yako kutaka kukuzuia wewe ni mbele kwa mbele ili uweze kushinda katika hayo yote.
Kwa nini ujasiri na uhodari?
• Ujasiri ili usiogope njiani;
• Uhodari ni kujua Neno, ni lazima ujue Neno ili uhodari wako uweze kutokea hata ukikutana na jambo uweze kutamka Neno na iwe sawa sawa na vile unavyotaka.
Mambo yoyote yatamanikayo ni halali yako sasa ni kazi yako wewe kuchagua kile unachokitaka, hakuna wa kukuzuia kwa sababu ni halali yako, Biblia inasema “mbingu na nchi ni mali ya Bwana” hii ina maana kuwa wewe ni wa Mungu na kila kilicho chake ni chako.
Mithali 8:18 “ Utajiri na heshima ziko kwangu, Naam, utajiri udumuo, na haki pia.” Pesa na heshima ni haki yako, sasa kwa nini wewe hauna? Kwa sababu hauna msingi wa kuvipata, hakikisha mapenzi yake unayafanya ili iwe msingi wako wa kupokea yale Mungu aliyokukusudia.

Add Comment